WAZIRI wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Mohamed Mchengerwa amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa jitihada zake kukuza michezo nchini.
Waziri Mchengerwa aliyasema hayo hivi karibuni, wakati akifunga mashindano ya gofu ya kumuaga aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo na Kumkaribisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda ulezi wa klabu ya gofu Lugalo.
Amesema majeshi yamekuwa na historia ya kutoa mchango mkubwa katika michezo na kwamba wachezaji wengi wanaoshinda mashindano mengi wanatoka kwenye majeshi.
Amesema kutokana na nidhamu iliyojengeka kwenye majeshi, ana imani kuwa jeshi lina uwezo wa kuanzisha timu na ikafanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesifu juhudi zinazofanywa na jeshi, katika kuanzisha klabu ya gofu na miundombinu ya mchezo huo, Dar es Salaam na Dodoma na kuruhusu raia kutumia.
Mwanzilishi wa klabu ya gofu ya Lugalo, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali, George Waitara amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Jenerali Mabeyo na kueleza kuwa ana imani kubwa na mlezi mpya wa klabu hiyo, Jenerali Mkunda.
Kwa Upande wake, Jenerali Mkunda ameahidi kuiendeleza klabu hiyo pamoja na klabu ya gofu ya JWTZ Ihumwa Dodoma.