Kabudi ahimiza utunzaji misitu

MBUNGE wa Kilosa, mkoani Morogoro, Profesa Palamagamba Kabudi  amewataka wananchi kutunza misitu.

Profesa Kabudi alisema hayo jumatano katika Kata ya Rudewa, wilayani humo mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2022, Sahili Geraruma.

Mwenge ulifika katika kata hiyo kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa maji.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya Sh bilioni 3.1  kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ndani ya jimbo hilo ukiwamo mradi wa maji wa Rudewa ambao umegharimu takribani Sh milioni 847.

Taarifa iliyotolewa mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ilisema lengo la mradi huo ni kutoa huduma ya maji mengi, safi na salama kwa saa 24 kwa wakazi wapatao 13,516 wa Kata ya Rudewa na kuongeza upatikanaji wa maji kwa wakazi hao kutoka asilimia 15 hadi kufikia 95.

Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Geraruma aliipongeza Wilaya ya Kilosa kwa kutekeleza ipasavyo mradi wa Maji wa Rudewa unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa).

Geraruma alisema hatua hiyo ni kuunga mkono sera inayosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kutekeleza dhamira yake ya kumtua mama ndoo kichwani.

“Ndugu zangu wana Rudewa, mwenge wa uhuru umefika hapa kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wetu wa maji unaotekelezwa na ndugu zetu wa Ruwasa, kwenye hiki kipengele cha maji Ruwasa mko vizuri, hongereni sana,” alisema Geraruma.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button