Kaburi la mtoto lafukuliwa, mwili, jeneza vyaibwa

WAKAZI wa Kitongoji cha CCM-Senta, Kijiji cha Lwamugasa wilayani Geita mkoani hapa wamekutwa na sintofahamu baada ya kaburi la mtoto aliyezikwa kukutwa limefukuliwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya tukio hilo juzi, baba wa mtoto, Dismas John (35) alisema mwanawe wa miaka miwili, alifariki Februari 15 na kuzikwa Februari 16, 2023 katika malalo ya kijiji hicho.

Alisema chanzo cha kifo cha mwanawe ni baada ya kuugua kwa siku mbili mfululizo, ambapo alifariki siku ya tatu wakiwa njiani kumpeleka kwenye matibabu katika kituo cha afya kilichopo mji mdogo wa Katoro.

“Tulienda kuzika katika malalo ya kijiji na baada ya hapo, tarehe 17 (Februari), ubalozi jirani na wao walipata msiba na kwenda malaloni, baada ya kufika eneo la malaloni walikuta kaburi lile limefukuliwa.

“Mwili na jeneza vyote havimo, liko wazi, mimi nilikuwa bado nipo nyumbani walinipigia simu, nikafika maeneo ya tukio kweli nikashuhudia mwenyewe, na wale watu waliokuwa wanazika pale walishuhudia.

“Baada ya hapo nilichukua hatua ya kuripoti serikali ya kijiji, nilianza na hatua ya balozi, tukawasiliana na mwenyekiti, ambaye hakuwepo ofisini akasema hilo jambo atalifuatilia,” alisema.

Mkazi wa Kijiji cha Lwamugasa, Masumbuko Anthony alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo limeibua taharuki kwani ni mara ya kwanza kutokea tukio la aina hiyo na hawaelewi ni nani aliyehusika.

Alisema taarifa walizipata baada ya baba wa marehemu kupigiwa simu naye kuwaarifu viongozi na majirani zake ambapo waliambatana kwenda kujiridhisha na walikuta tukio hilo ni la kweli.

Naye Isack William alisema: “Nilifika kwenye tukio, nilichokiona ni kaburi limechimbwa, mashada yamewekwa pembeni, tukaulizana jeneza lipo au halimo, tukakosa namna ya kufanya tukapigia simu polisi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lwamugasa, Musa Songoma alisema uongozi wa kijiji ulifika eneo la tukio na kuona ingawa hawakuweza kufukua mpaka chini kujua kama jeneza lipo ama la na wanasubiri ripoti ya Jeshi la Polisi.

HabariLEO inaendelea na juhudi za kulitafuta Jeshi la Polisi kwa ajili ya kupata taarifa za uchunguzi.

Habari Zifananazo

Back to top button