Kada CCM awakingia kifua viongozi wastaafu
KADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa mjini Iringa, Mugabe Kihongosi amempongeza Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kujali viongozi wastaafu akisema viongozi hao ni muhimili wa taifa na wanapaswa kuendelea kutoa ushauri na mchango wao katika uendelezaji wa nchi.
Aidha ampongeza Rais kwa anavyoendelea kuwaamini na kuwateua vijana kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na katika chama ukiwemo uteuzi wa hivikaribuni wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Paul Makonda.
Akizungumza na wanahabari mjini Iringa leo, Kihongosi alisema amelazimika kutoka hadharani na kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari ili kutoa pongezi zake kwa mheshimwa Rais kwa namna anavyoyatumia makundi hayo mawili kusukuma ipasavyo gurudumu la maendeleo.
“Tuliona ziara ya Rais aliyoifanya kwa nyakati tofauti kuwatembelea viongozi wakuu wastaafu wakiwemo marais na mawaziri wakuu wastaafu. Tuna amini kuna ushauri na busara kubwa anabeba kwa kupitia viongozi hao na zinamsaidia katika kuliongoza Taifa hili lililobarikiwa kwa amani,” alisema.
Kihongosi aliwapa sifa viongozi hao akisema ni sawa na wazazi hivyo ni vizuri; “Tukawaenzi, tukawaheshimu na tukafuata ushauri wao katika masuala ya kiuongozi na kitaifa pia pale inapohitajika.”
Akiwasihi viongozi hao kutovuka mipaka ya ushauri na kuchangia, Kihongosi alisema halitakuwa jambo la busara kama watataka kufanya mambo hayo kama viongozi ambao bado wako madarakani.
Akipokelewa Makao Makuu ya CCM jijini Dodoma hivi karibuni, Makonda aliwazungumzia wastaafu hao akisema sio utaratibu kila siku kuongeaongea huku akiwashauri watulie, walee familia zao na kwamba wakihitajika kwa ajili ya kazi yoyote ile wataitwa.
Akizungumzia nafasi za vijana Kihongosi alisema Rais Samia amewaamini na kuwapa nafasi mbalimbali nyeti za uongozi ikiwa ni pamoja na wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa wilaya na mikoa, naibu waziri na mawaziri akitarajia kwamba watafanya kazi zao kwa kuzingatia katiba, sharia, kanuni na miongozo mbalimbali.
“Yote hiyo ni kutuamini vijana kwamba tunaweza kuwa viongozi. Rai yangu kwa vijana ni vizuri nafasi hizi tukazitumia vizuri kwa kuleta matunda makubwa ambayo Mheshimwa Rais anatarajia kutoka kwetu,” alisema.
Wakati huo huo kada huyo ameipongeza serikali ya Rais Samia kwa namna inavyotekeleza kwa kasi kubwa Ilani yake ya uchaguzi kupitia sekta mbalimbali za maendeleo kama afya, elimu, nishati, miundombinu na maji.
Alisema kasi hiyo inaihakikishia CCM ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwakani wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Amezungumzia pia vyama vya upinzani akisema vina mchango mkubwa katika kuionesha njia serikali ya CCM ili itekeleze Ilani yake kwa ufanisi mkubwa zaidi.