WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameitaka Bodi Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini ‘LATRA’ kushirkiana na wadau mbalimbali katika sekta ya usafirishaji ili kuimarisha mahusiano katika sekta hiyo.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo leo Julai 11 , 2023. Dar es salaam wakati akizindua bodi mpya ya mamlaka hiyo (LATRA) na kuainisha sababu ya changamoto zinazojitokeza katika sekta hiyo pamoja na kuweka bayana njia za kutatua changamoto hizo.
“Binadamu yeyote anataka asikilizwe kwahiyo ninaomba sana bodi hii muwe na vikao vya mara kwa mara na hawa wadau mfano wamiliki wa mabasi, kaeni nao muwasikilize changamoto zao, wakati mwingine inatokea hata migomo lakini mngekuwa mnakaa mnaweza kufanya haya yasitokee” amesema Mbarawa
Prof Mbarawa pia ameitaka bodi hiyo kuhakisha wanashughulikia malalamiko ya wafanyakazi pamoja na wadau lakini pia kutoa mafunzo kwa pande hizo.
“Hakikisheni mnashughulikia malalamiko ya wafanyakazi, na wadau pamoja na kuboresha huduma kwa wateja, Wapeni fursa wakajionee, leo mtu anashughulika na Tazara lakini hapajui wala hajui uendeshaji wake, wapelekeni wakaone itasaidia wao kufanya kazi kwa ufasaha zaidi” amesema Mbarawa
Katika hatua nyingine Mbarawa ameitaka bodi hiyo kuishauri wizara ya Ujenzi na Uchukuzi juu ya safari za mabasi hasa safari za saa tisa usiku kwa kufanya uchambuzi yakinifu.
“Fanyeni uchambuzi wenye uhakika alafu mje mtu shauri, ninaamini mkifanya hivyo mtaasaidia sana hata kupunguza ajali za barabarani, mkishafanya uchambuzi wenu njooni na suluhisho la nini kifanyike mtakuwa mmesaidia pakubwa” amesema Mbarawa
Mkurugenzi mkuu wa Latra CPA Habibu Suluo pamoja na mwenyekiti mpya wa bodi hiyo Prof. Ahmed Mohamed Ame wamesema lengo lao ni kuendelea kufanya kazi kwa ubora ili kuendelea kuipa hadhi mamlaka hiyo.
Comments are closed.