Kagame aondoka, maagizo yafanyiwa kazi

RAIS wa Rwanda, Paul Kagame amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili na kuondoka nchini huku mawaziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na Tanzania wakianza kujipanga kutekeleza maagizo yaliyotolewa na viongozi wa mataifa hayo.

Akizungumza jana katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam wakati akimsindikiza Rais Kagame kuondoka nchini, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema tayari wameshaanza kutekeleza maagizo ya viongozi hao.

“Mengi yalishasemwa na viongozi wetu (Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Paul Kagame), walipokutana jana (juzi) Ikulu, walitoa maelekezo mahususi kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa haya mawili wakutane mara moja na hivi mnavyotuona tumekutana na tunapanga jinsi ya kutekeleza mipango ya utekelezaji,” alisema Dk Tax.

Alisema viongozi hao walibainisha wazi maeneo ya kufanyia kazi kuwa ni pamoja na miundombinu, Tehama na uendelezaji wa viwanda. Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dk Vincent Biruta akizungumza uwanjani hapo mara baada ya Rais Kagame kuondoka alisema wamekutana na Dk Tax kuzungumza jinsi ya kutekeleza yale yaliyoafikiwa na viongozi wa mataifa hayo.

Akiwa nchini Rais Kagame pamoja na mwenyeji wake Rais Samia walikubaliana kuimarisha masuala mbalimbali ya ushirikiano hususani kwenye sekta ya biashara, miundombinu ya bandari na mingine, mradi wa umeme wa Rusumo pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.

Viongozi waliomsindikiza Kagame wakati akiondoka nchini kurejea Rwanda hapo jana ni pamoja na Dk Tax, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu- Zanzibar, Jamal Kassim Ali na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Wengine waandamizi wa serikali waliomsindikiza ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Samwel Shelukindo, Balozi wa Rwanda nchini, Meja Jenerali Charles Karamba na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Naimi Aziz.

Rais Kagame alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini na aliwasili juzi na kuondoka jana baada ya kukutana Ikulu na mwenyeji wake Rais Samia ambapo walifanya mazungumzo kisha kuzungumza na waandishi wa habari mambo waliyojadiliana na kuafikiana.

Hii si mara ya kwanza Rais Kagame kufanya ziara nchini kwani aliwahi kuzuru mwaka 2018 na baadaye mwaka 2019 alikuja tena. Ziara ya Rais Kagame inafuatia ziara ya Rais Samia aliyoifanya nchini Rwanda mwaka 2021.

Habari Zifananazo

Back to top button