Kagera wapo tayari madarasa kidato cha kwanza

Kagera wapo tayari madarasa kidato cha kwanza

UJENZI wa vyumba vya  madarasa  pamoja na uwekaji wa viti kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2023  mkoani Kagera umefikia asilimia 85.

Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila kwa wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), imewahakikishia kuwa ifikapo Januari muda wa wanafunzi kuanza kupokelewa shuleni, miundombinu ya madarasa itakuwa imekamilika, hivyo jukumu lao kuhakikisha watoto wote waliochaguliwa wanajiunga na kidato cha kwanza bila kikwazo.

Alisema ujenzi huo wa madarasa pamoja na ununuzi wa viti unagharimu kiasi cha shilingi mil 514, ambayo ilitolewa na Rais Dk  Samia  Suluhu Hassani,  ikiwa ni muendelezo  wa kuinua elimu nchini kwa kujenga miundombinu bora.

Advertisement

Alisema Rais Samia amefanya mkubwa katika mkoa wa Kagera, ikiwa ni pamoja na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo, ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022  jumla ya Sh Bilioni 79.5 zimetumik kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Kagera.

“Fedha hizo ni nyingi na zinahitaji usimamizi mkubwa, hivyo naahidi kuwa tutaendelea kusimamia fedha hizo kwa nidhamu ya juu kwa maslahi ya mkoa na taifa kwa ujumla,” alisema Chalamila.

Amesema kuwa kwa  mwaka wa fedha 2022/2023 hadi Septemba 2022, tayari mkoa wa Kagera umeshapokea Sh bilioni 21.0, ambapo kati ya fedha hizo nyingi zilikuwa ni kwa ajili ya sekta ya elimu, afya na miradi mingine .

Kikao hicho kilijadili ajenda mbalimbali za maendeleo kwa mwaka 2022/2023, ambapo Chalamila aliwataka watumishi wote na watendaji katika Halmashauri kuhakikisha wanasimamia miradi hiyo kwa ukaribu na kuhakikisha inakamilika kwa kuonyesha thamani ya fedha iliyotumika

1 comments

Comments are closed.