Kahama waonywa mawakili vishoka
WANANCHI wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga wameonywa kuwa makini na mawakili, kwani baadhi yao hawana sifa na wanaishia kuchukua fedha bila kuwasaidia chochote mahakamani.
Hatua hiyo inatokana na kuwepo wimbi la baadhi ya watu wanaojitambulisha kuwa ni mawakili na kuchukua fedha kutetea wananchi, wakati mfumo wa mahakama hauwatambui.
Kauli hiyo imesemwa leo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Edmund Kente na kueleza kuwa kuna kila sababu wananchi kuwa makini wanapotaka kupewa msaada wa kisheria, kwani mawakili hao hawaingii mahakamani na wanaishia nje, kiasi cha kuwafanya wananchi kukosa msaada.
Pia amesema mfumo wa JSDS, ambao unaratibu mashauri yote na uendeshaji wa kesi kwa njia ya mtandao, umepunguza idadi ya kesi kwa kiasi kikubwa.
Amesema mwaka huu wa 2022 walianza na kesi 252, lakini tayari kesi 189 zimeshasikilizwa na kwamba zilizobaki hadi kufikia Desemba mwaka huu zitakuwa zimesikilizwa zote.