Kairuki akutana na ujumbe wa China

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki amekutana na ujumbe kutoka Jamhuri ya Watu wa China ambao pamoja na mambo mengine wamajediliana namna ya kushirikiana katika maeneo kadhaa yakiwemo ya ushirikiano kwenye serikali za mitaa na maendeleo ya kilimo.

Pia kujenga uwezo na maendeleo ya rasilimali watu katika maeneo ya Utawala, Elimu, Afya, maendeleo ya miundombinu vijijini na maendeleo ya miundombinu na ushirikiano wa uwezo wa uzalishaji utakaoiwezesha Tanzania kuongeza tija na kupata soko la China.

Ujumbe huo ambao umeongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya 13 ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Watu wa China na Rais wa Chama cha Kirafiki kati ya watu wa China na Afrika, Dkt. Li Bin.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kairuki alisema ushirikiano wa serikali za mitaa kati ya China na Tanzania utawezesha pande zote mbili kubadilishana uzoefu katika mapambano dhidi ya umaskini katika ngazi ya chini.

“Tumekuwa tukijifunza kutokana na uzoefu wa mafanikio wa China katika kupunguza umaskini na maendeleo, tukitumai siku moja tutaondoa kabisa umaskini miongoni mwa watu wetu kwa kuimarisha ushirikiano wa kirafiki na kunufaishana kati ya China na Afrika.”

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi za Afrika ambazo zimerekodi mafanikio ya kutia moyo katika kupambana na umaskini katika miongo miwili iliyopita.

“Hata hivyo kazi kubwa zaidi inatakiwa kufanywa ili kufikia Ajenda ya Afrika 2063 pamoja na kufikia malengo ya kumaliza umaskini, kulinda ustawi wa jamii kama sehemu ya ajenda mpya ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030. Kwa hiyo, tuna kazi ya haraka ya kufikia kupunguza umaskini na maendeleo.”

“Tuna matumaini kuwa kupambana na umaskini si jambo lisilowezekana kwa sababu tuna fursa ya kushirikiana na rafiki na mshirika wetu China, kupigana na kushinda vita hivi.”

Kairuki aliongeza: ”nia yetu ni kuimarisha ushirikiano wetu wa serikali za mitaa, tumejitolea kudumisha mawasiliano ya hali ya juu na kuimarisha uaminifu wa kisiasa wa pande zote.”

Kwa upande wa Li Bin alitumia fursa hiyo kumualika Mhe. Angellah kwenye kongamano la China na Afrika kwenye masuala ya Serikali za Mitaa litakalofanyika mwaka 2024.

Katika mualiko huo pamoja na ujumbe atakaoambatana nao wataandaliwa zaira ya kutembelea Serikali za Mitaa za China ili kujionea na kujifunza namna walivyojikwamua katika kuondokana na umasikini.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button