Kairuki apokea mapendekezo mikopo ya 10%

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Rais,  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki

WAZIRI  wa Nchi, Ofisi ya Rais,  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki amepokea taarifa ya mapendekezo ya  Kamati Maalumu ya kitaifa ya kupitia utaratibu mpya wa usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa makundi maalumu ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Kutokana na hilo, Angellah aliamuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo na wataalamu wake kupitia mapendekezo hayo ndani ya  siku saba.

Akizungumza jana mara baada ya kupokea taarifa hiyo wilayani Kibaha mkoani Pwani, alisema, “ nitoe siku saba kwa Katibu Mkuu na wataalamu wetu kupitia mapendekezo yote kwa kina, tuweze kuona faida ya kila pendekezo na kila mfumo pamoja na gharama zitakazotumika katika mfumo huo, vile vile maboresho ya kiutawala, kiutendaji na usimamizi.”

Advertisement

Alisema mapendekezo ya kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa wakati akipokea  taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2021/2022 ya kuboreshwa kwa mfumo wa utoaji, utaratibu, usimamizi na urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10.

Alimtaka Katibu Mkuu na timu ya wataalam kupitia mapendekezo yote na kuja na uchambuzi wa kina wa mfumo bora utakaokuwa na maboresho na kuleta tija kwa makundi yaliyokusudiwa kulingana na maelekezo ya Rais.

Angellah aliipongeza kamati hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Samwel Wangwe kwa kufanya kazi kwa umakini na kushiriana na wadau pamoja na taasisi za kifedha na kutoa mapendekezo ya mwongozo utakaotumia kuratibu na kusimamia utoaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10.

Ikumbukwe kuwa Aprili 13, mwaka huu Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliagiza halmashauri zote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo kwa makundi maalumu kuanzia Aprili hadi Juni, 2023 wakati serikali inajipanga kuweka mfumo mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *