UKIPIGA hapokei, wala ujumbe hajibu. Wengi wa watu wake wa karibu humlalamikia kuwa amebadilika.
Mmoja alinukuliwa: “Amekuwa mwepesi hata mbele ya hadhara kushambulia waandishi, wachezaji, viongozi na wengine wa rika makamo ya wazazi wake”.
Hivi sasa, mengi ayasemayo katika mikutano na waandishi wa habari yamejaa dhihaka, mbwembwe kupitiliza, maelezo yasiyo ya lazima. Almuradi tujuwe naye sasa ni fulani.
Anakumbukwa kwa mengi mazuri na hata makucha yake sasa hayajafuta hata theluthi ya weledi, uzalendo, mapenzi yake kwa mpira wa miguu na sanaa kiujumla.
Kwa wengi anafahamika kama kijana mwanamapinduzi wa uchambuzi wa soka uliohusisha taaluma yenyewe, kwakuwa ana leseni ya mwanzo ya ukocha. Pia uwezo wake wa kujenga hoja, na kutetea hoja hiyo kwa fikra tunduizi.
Ni yeye ambaye ilikuwa ni ngumu kutofuatilia amesema nini punde baada ya mitanange ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mwisho huwa na kibwagize aliyekipa anuani n.b wengi sasa wanaiga kutoka kwake.
Lakini waneni hunena ukitaka kujua mwendo wa mjinga mpe kilemba uone, huwenda kukosa ‘cheo’ huficha uhalisia wa mtu kama wengi wa watu hushuhudiwa.
Wengi tusichojua kuhusu yeye, pia ana kipaji cha kuigiza na hata ndoto zake za awali zilikuwa aje kuipeperusha Tanzania kama hayati Steven Kanumba (fuatilia mahojiano yake na online fulani ya mwenye cheo kama chake shirikishoni utanielewa).
Sasa sijui huyu wa sasa anaigiza ama yule ndiye muigizaji? Muda bado upo kaka, hujachelewa. Usiwe katika mkumbo wa mfano wa vijana wanaofanya vijana wenzao tutukanwe sababu ya vyeo. Usibadilike kama yule Zuwena aliyeimbwa na Diamond.
Jitafakari.