MAKAMU wa Rais wa zamani wa Kenya, Kalonzo Musyoka amesisitiza umuhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kurejesha haraka matumizi ya sarafu moja ili kufungua milango ya kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama.
Kuhusu hoja hiyo, mmoja wa wawakilishi wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Mashaka Ngole, amesema kupatikana sarafu ya pamoja kutakuwa njia sahihi ya nchi wanachama wa EAC kufungua mipaka ya kibiashara pasipo vikwazo.
“Hii ni kwa kuwa sarafu hiyo itatumika katika nchi zote na kiwango kitakuwa sawa; hatua hii itasaidia wananchi kuwa huru zaidi katika biashara zao,” alisema Ngole.
Katika mazungumzo na HabariLEO Afrika Mashariki kwa nyakati tofauti jijini hapa baada ya wabunge wapya wa EALA wanaowakislisha nchi zao kuapishwa, Kalonzo alisema matumizi ya sarafu moja kwa EAC yataongeza kasi na nguvu ya msikamano baina ya nchi za jumuiya hiyo na kufungua fursa zaidi za kiuchumi.
Kufanyika kwa jambo hili kutazifanya nchi za EAC yaani Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutumia sarafu moja yenye thamani sawa katika nchi zote.
“Kuongezwa kwa DRC katika EAC kunasababisha msukumo mkubwa wa kiuchumi katika nchi wanachama,” alisema Kalonzo.
Akaongeza: “Wabunge wa EAC wanapaswa kufanya kazi zaidi kuziunganisha nchi zote za EAC na kufungua mipaka ili kusiwepo vikwazo na wananchi wa jumuiya hii wawe na sawa na uhuru wa kibiashara.”
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, aliwasihi wabunge wa EALA kuendeleza mtangamano ili kukuza biashara ndani ya EAC.
Dk, Tax alisema umoja ni muhimu kuimarisha umoja ili kwenda pamoja katika nyanja mbalimbali hususani programu za kuendeleza miundombinu inayoakisi uchumi wa kijiografia kwa nchi wanachama wa EAC.
Aprili mwaka huu, Mwenyekiti wa Wabunge wa EALA, Adam Kimbisa alinukuliwa akisema hatua ya kutumia sarafu moja ni muhimu katika kurahisisha biashara kwani itasaidia kuondokana na utaratibu wa kubadili fedha kila unapovuka mpaka kutoka nchi moja ya EAC kwenda nchi nyingine.
“Majadiliano ya Itifaki ya Umoja wa Fedha yalikamilika mwaka 2013. Nchi wanachama zilikubaliana kuwa na kipindi cha maandalizi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2014 na inatarajia kukamilika ifikapo 2024,” alisema.
Akaongeza: “Baraza la mawaziri litakutana hivi karibuni kuongeza muda kwa sababu bado mchakato haujafika katika hatua ambayo kufikia mwaka keshokutwa (2024) itakuwa imekamilika.”