Kamala: Afrika muhimu kwa usalama

 MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango leo anatarajiwa kumpokea Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) mkoani Dar es Salaam.

Serikali kupitia kwa Msemaji wake mkuu, Gerson Msigwa imemkaribisha kiongozi huyo na imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha diplomasia.

“Karibu Tanzania Mhe. Kamala Harris, Makamu wa Rais wa Marekani. Asante Mhe. Rais Dkt. @SuluhuSamia kwa kuimarisha diplomasia na uhusiano wetu na Mataifa makubwa Duniani. Tupo tayari kumpokea Makamu wa Rais wa Marekani…,” ameandika Msigwa katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa twitter.

Kamala Harris ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo nchini Marekani, anakuja nchini akitokea Ghana na akiondoka nchini anatarajiwa kwenda Zambia.

Baada ya kufika Ghana, Machi 26, mwaka huu, kupitia ukurasa wake wa twitter alieleza kuwa ni heshima kwake kuwa barani Afrika na kwamba nchi katika bara hilo ni muhimu kwa usalama wa dunia.

Alieleza kuwa akiwa barani humo anatarajia kukutana na viongozi, vijana na wajasiriamali wanapofanya kazi pamoja kuwekeza katika ubunifu barani humu.

“Safari yangu ya wiki moja barani Afrika ni kutambua kwamba nchi za Afrika ni muhimu kwa mafanikio ya dunia na ulinzi na mawazo na ubunifu wao vina manufaa kwa dunia,” ameandika kwenye ukurasa wake wa twitter.

Katika ukurasa huo, ametoa orodha ya nyimbo 25 anazosikiliza akiwa kwenye ziara hiyo za wasanii wa Tanzania, Ghana na Zambia ukiwamo Mahaba wa Ali Kiba, Sawa wa Jay Melody, Single Again wa Harmonize, Utaniua wa Zuchu na Shetani wa Mbosso akiwashirikisha Alfa Kat na Costa Titc.

Rais Samia anatarajia kumpokea kiongozi huyo Ikulu Dar es Salaam kesho na baada ya mazungumzo yao, kiongozi huyo anatarajiwa kuweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa, kuashiria kuwakumbuka waathirika wa mabomu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998.

Pia kesho Kamala anatarajiwa kutembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association, kukutana na wajasiriamali vijana na baadaye atashiriki futari iliyoandaliwa na Rais Samia katika Ikulu ya Magogoni.

Juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema Kamala anakuja kwa mwaliko wa Rais Samia walipokutana Washington D.C Aprili mwaka jana wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Marekani.

Pia alisema kiongozi huyo anakuja kutekeleza ahadi iliyotolewa Desemba mwaka jana na Rais wa Marekani, Joe Biden wakati wa mkutano wa kilele kati ya Marekani na viongozi wa Afrika.

 

Habari Zifananazo

Back to top button