Kamala Harris awakumbuka wahanga wa mabomu

MAKAMU wa Rais wa Marekani Kamala Harris ameweka shada la maua katika mnara wa kumbukumbu ya mabomu yaliyolipuka kwenye balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998 huku akiahidi kuwa Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kupiga vita ugaidi.

Kamala ameweka shada la maua katika mnara huo ikiwa ni miaka 25 imetimia tangu tukio hilo litokee.

Akizungumza leo Machi 30, 2023 na waliokuwa wafanyakazi nane wa Ubalozi wa Marekani walionusurika katika shambulizi la kigaidi lililotokea usiku wa kuamkia Agosti 7, 1998 Kamala amesema serikali yake itashirikiana na Tanzania kupinga ugaidi ili ardhi ya Tanzania na Marekani iwe sehemu salama kwa wananchi wa nchi zote mbili.

Advertisement

“Marekani imesimama na Tanzania katika kuomboleza vifo vya Watanzania 11 ambao walikuwa watumishi wa Ubalozi wa Marekani, na itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika kutokomeza ugaidi duniani.”Amesema

Balozi wa Marekani wakati shambulizi hilo likifanyika mwaka 1998 Charles Stith amesema ingawa lilikuwa tukio la kuogopesha anaishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Mkapa kwa ushirikiano mkubwa alioutoa kukabiliana na tukio hilo.

Amesema sababu ya kujenga mnara wa kumbukumbu ya tukio hilo ni pamoja na kuwaenzi Watanzania 11 waliokufa na wale wote waliojeruhiwa pamoja na kutunza urafiki uliopo kati ya Tanzania na Marekani katika nyanja mbalimbali.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Noel Lwoga amesema ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani umechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi kubwa anayoifanya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha diplomasia na ushirikiano na mataifa duniani.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *