Kamati kutatua kero za wafanyabiashara yaundwa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ameunda Kamati ya watu 14 kushughulikia kero ya wafanyabiashara Kariakoo huku akiagiza kusitisha kanuni ya tozo ya stoo.

Akizungumza kwenye kikao cha Wafanyabiashara kilichofanyika Mnazimoja leo Mei 17,2023  amesema kamati hiyo itazungumza nchi nzima kukusanya kero za wafanyabiashara.

Kamati hiyo ina wajumbe 14  ambao wajumbe saba ni kutoka Serikalini na wajumbe wengine saba ni wawakilishi wa wafanyabiashara akiwemo Fred  Ngajiro‘Vunja Bei’.

Advertisement

Majaliwa akizungumza na wafanyabiashara hao amesema, kodi ya stoo  inayotozwa na Viwanda na Biashara haina mgogoro ila kanuni zake zina mianya ambayo zinaleta kero kubwa kwa wafanyabiashara.

“Kodi za stoo, kama inayotozwa na Wizara ya Viwanda na Biashara haina mgogoro kwanini hii ina mgogoro kuna tatizo mahala, Sheria iliyopo sio mbaya inawezekana kanuni ndio zinamianya ya kero hivyo kanuni hizo nazisitisha,”amesema Majaliwa

Aidha, amesisitiza agizo lake la kuondoa kikosi kazi alilolitoa juzi Mei 15, 2023   linabaki  palepale kwani ilikuwa inafanywa na watu wenye tamaa za maisha akisisitiza kodi itakusanywa na watumishi wa TRA na watabanwa kulingana na maadili yao.

“Kuna suala la Jeshi la Polisi kwenda kukusanya kodi linaleta mkanganyiko kazi ya jeshi la Polisi ni kulinda raia na mali zake sio kukusanya kodi.”Amesema

Majaliwa pia amewataka wafanyabiashara ambao mizigo yao imekamtwa wawasilishe madai yao kwa kamati aliyoiteuwa ili iweze kushughulikiwa na waweze kurudishiwa mizigo yao.

Kufuatia maagizo hayo, Majaliwa akiwa anashangiliwa na wafanyabiashara aliwasihi kufungua biashara zao wakati kero hizo zinashughulikiwa.

“Nawaomba sana wafanyabiashara wetu mjue soko letu hili ni la Kimataifa, wale wateja walioondoka muwarudishe inaumiza kusikia vitenge vinashuka  hapa kwenda Uganda na baadae kurudi nyuma nyuma, nawaomba na nawasihi mfungue…mtafungua? Alihoji na wafanyabiashara kuitikia ‘Ndioooo’

/* */