Kamati nne zaundwa kuijenga jumuiya ya wazazi Iringa

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imeunda kamati nne zitakazosaidia kuiongezea mvuto na nguvu ya kiuchumi katika mkakati wake unaolenga kujiondoa na biashara ya mazoea iliyoifanya kwa miaka yote ionekane kama taasisi ya wazee.
Akizitaja kamati hizo wakati zikizinduliwa leo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Fadhili Ngajilo alisema zinaundwa kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
“Tumeweka historia, hatujawahi kuwa na kamati za aina hii tangu jumuiya hii ianzishwe. Niishukuru kamati yangu ya utekelezaji kwa kuja na ubunifu huu. Matarajio yetu baada ya kufanikisha jukumu hili kwa ngazi ya mkoa, tutashuka pia kwa ngazi ya wilaya,” alisema.
Kamati hizo ni pamoja na ya Elimu, Malezi Afya na Mazingira ambayo ni kamati mama kwani ndiyo inayobeba majukumu ya msingi ya jumuiya kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo yake.
“Kwa kupitia kamati hii yenye wajumbe 19 tunakwenda kuhakikisha tunafuatilia changamoto zilizoko katika maeneo ya elimu, mazingira, afya na malezi na kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa mamlaka zingine wa namna ya kutatua changamoto hizo,” alisema.
Aliitaja kamati nyingine kuwa ni ya hamasa aliyosema itakuwa na jukumu kubwa la kuhamasisha wananchi kujiunga na CCM na jumuiya hiyo kwa kufanya ziara za mara kwa mara za kuwafikia wananchi kupitia mashina ya chama hicho mkoani kote.
“Kwa kupitia kamati hii tunakwenda kuachana na ziara za kuishia makao makuu ya wilaya na kata, sasa tutakwenda kufanya kazi katika ngazi ya chini kabisa hatua tunayoamini itaiongezea jumuiya mvuto,” alisema na kuongeza kwamba kamati hiyo ina wajumbe 23.
Kamati nyingine ni ya Miradi na Uwekezaji aliyosema itakuwa na wajibu wa kubuni miradi na kuwekeza ili kuifanya jumuiya iwe na nguvu kubwa kiuchumi
Nyingine ni kamati ya Fedha na Uwezeshaji itakayokuwa na wajibu wa kusimamia miradi yote itakayoanzishwa.
“Mbele yetu kuna mradi wa kujenga vibanda zaidi ya 80 vya biashara mjini Iringa. Vibanda hivi vitajengwa na Kamati ya Miradi na Uwekezaji na vikikamilika vitasimamiwa na kamati ya Fedha na Uwezeshaji,” alisema.
Alisema miradi mingine ambayo jumuiya hiyo inafikiria kuwa nayooni pamoja na kuwa na nyumba za kulala wageni zitakazojulikana kama wazazi lodge, kilimo, burudani, chama cha kuweka na kukopa (Saccos) na biashara zingine.
Awali Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Iringa, Daima Nyoni alisema milango ya jumuiya hiyo kwa ajili kupokea wanachama ipo wazi na sifa kuu ni kuanzia miaka 18 na kuendelea na sio wazee pekee kama inavyofikiriwa na wengi.
Alisema jumuiya hiyo imechoka kuwekwa nafasi ya tatu baada ya jumuiya ya vijana na wanawake wa chama hicho na sasa inataka kuzitumia kamati hizo kuifanya iwe ya kwanza na yenye nguvu.
Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Rukia Mkindu alisema uhai wa chama hicho unatategemea namna viongozi na wanachama wake wanavyotimiza wajibu wao katika kukiimarisha chama hicho.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa, Salvatory Ngelela alisema wamepokea kwa mikono miwili ubunifu wa jumuiya hiyo na watahakikisha wanashirikiana na chama na wadau wengine kufikia malengo yake.