Kamati ya Bunge yaridhishwa maji yanavyoboresha jamii

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imetembelea miradi ya maji katika vijiji vya Itagutwa, Nyabula, Mlanda na Masaka wilayani Iringa na kupongeza jinsi huduma hiyo inavyobadilisha maisha na kuboresha jamii katika maeneo hayo.

Katika vijiji hivyo, upatikanaji wa maji safi ulikuwa changamoto ya muda mrefu kwa wakazi wake huku wanawake na watoto wakitumia saa kadhaa kila siku kutafuta maji kutoka vyanzo vya mbali, vingi vikiwa vichafu na visababishi vya magonjwa huku vikupunguza fursa za ukuaji wa uchumi.

“Ukosefu wa maji ya kuaminika pia uliathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo na afya ya mifugo,” alisema Diwani wa Kata ya Masaka, Mathew Nganyagwa mara baada ya kamati hiyo ikiwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi kutembela bwawa la Masaka lililojengwa kwa zaidi ya Sh Bilioni 1.7 na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (RBWB).

Bwawa hili lenye urefu wa zaidi ya kilometa 1.5 litawawezesha wananchi wa Masaka kupata miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, mabirika ya kunyweshea mifugo na maji safi na salama.

Naibu Waziri wa Maji alimpa miezi mitatu Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Iringa Mhandisi Exaud Humbo kuhakikisha visima vitano vya maji katika kijiji hicho cha Masaka vinapata vituo vya kuchotea maji ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama.

Ikiwa katika mradi wa Nyabula-Mlanda kamati ilipokea taarifa mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha lita 360,000 za maji huku mahitaji ya watu zaidi ya 17,800 wa vijiji hivyo vya Nyabula na Mlanda ikiwa ni lita 150,000.

Katika kijiji cha Itagutwa kamati hiyo ilitembelea mradi wa maji Itagutwa na kujionea kazi zilizofanyika zikiwemo za ulazaji mabomba wa umbali wa kilometa 12.75 , Ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji pamoja na ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 75,000.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni tiba ya utatuzi wa changamoto za upatikanaji wa maji katika vijiji hivyo na baadhi ya vitongoji kwenye vijiji jirani.

Kiswaga alizungumzia uharibifu wa mazingira unavyozidi kuongezeka duniani huku akiwataka wananchi wa vijiji hivyo kumuunga mkono Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika dhamira yake ya kutunza mazingira na kumtua mama ndoo.

“Tumepita katika vijiji hivyo na tumeona wanawake na watoto hawatembei tena umbali mrefu kutafuta maji hivyo kuwa na muda zaidi kwa shughuli za kipato, elimu na ushiriki wa mambo ya kijamii,” alisema Ritta Kabati, mjumbe wa kamati hiyo.

Kabati ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa alisema upatikanaji wa maji katika vijiji hivyo utavutia uwekezaji na fursa za maendeleo, biashara ndogo zitastawi, na miradi mipya kama vile shule na vituo vya afya itajengwa kwa urahisi na hivyo kuboresha ustawi wa wananchi.

Naye Mbunge wa Nyasa, Mhandisi Stella Manyanya amepongeza miradi ya maji akisema imepunguza magonjwa yanayosababishwa na maji machafu, ikiruhusu watu kuishi maisha yenye afya na furaha huku shughuli za kilimo na mifugo zikiongezeka.

Mhandisi Mahundi alisema wizara inaendelea na jitihada ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote na akahimiza usimamizi endelevu wa maji na vyanzo vyake kwa maendeleo ya jamii na taifa.

“Mafanikio ya miradi ya usambazaji wa maji hayabadilisha tu maisha ya wananchi, bali pia yamehamasisha vijiji kuchukua hatua kama hizo kuzalisha mabadiliko chanya katika maeneo yao,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button