KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama imeipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kutafsiri kwa vitendo maono yake.
Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Vita Kawawa walisema hayo wakati wa ziara kutembelea miradi ya kikanda ya barabara ya EAC katika mikoa ya Dodoma, Manyara na Arusha.
Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ilieleza kuwa ziara hiyo iliratibiwa na wizara hiyo na kutoa fursa kwa kamati kuona baadhi ya miradi ya EAC.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ziara hiyo pia ililenga kuonesha namna Tanzania inavyoshirikiana na Sekretarieti ya EAC na nchi wanachama kutekeleza miradi hiyo, kuanzia kufanya uchambuzi yakinifu na baadaye kutafuta fedha za utekelezaji.
Wajumbe walielezwa kuwa Tanzania imepakana na nchi tano za EAC; Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na katika nchi zote hizo kuna miradi ya barabara ya kuiunganisha Tanzania na nchi hizo.
Miradi michache ambayo ipo katika ujenzi ni barabara ya kutoka Kabingo, Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilometa 260 inayounganisha Tanzania na Burundi.
Barabara ya kutoka Tanga, Pangani, Saadani hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 256 inayounganisha Tanzania na Kenya. Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha pia daraja la Pangani la mita 500.
Kwa upande wa Tanzania na Uganda, kuna mradi wa barabara ya Mutukula, Kyaka, Kasulu hadi Benaco yenye urefu wa kilometa 124 na Bugene, Burigi, Chato hadi Kasulo yenye urefu wa kilometa 68.
Wakikagua barabara ya kikanda ya Arusha, Namanga, Athi River na Barabara ya Mzunguko ya Arusha, wajumbe walieleza namna ujenzi wa barabara hizo unavyounganisha nchi za EAC na kuchochea biashara, mwingiliano wa watu ili kuimarisha mtangamano.
Wajumbe wa kamati hiyo ambao pia walitembelea Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Namanga, walisikiliza mada kutoka kwa Mkurugenzi wa Miundombinuya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Eliabi Chodota.
Mada hiyo pamoja na mambo mengine ilieleza miradi mingine inayotekelezwa kwa uratibu wa EAC katika sekta za usafiri wa anga, reli, majini; hali ya hewa na nishati katika nchi wanachama.