Kamati ya Bunge yataka samani ATC

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imetoa rai kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani  ili kuwezesha wanafunzi wanapoanza muhula mpya wa masomo  katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC)wajifunze kwenye maabara mpya.

Rai hiyo imetolewa Jumapili na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo wakati walipotembelea chuo hicho kujionea umaliziaji wa jengo la madarasa, maabara na ofisi za wafanyakazi.

Alisema wizara hiyo itoe fedha kwa ajili ya ununuzi wa samani katika jengo hilo ili kuwezesha wanafunzi watakapofungua kuanza kutumia jengo hilo lenye madarasa na maabara za kisasa zaidi.

Alisema awali serikali ilitoa Sh bilioni 1.7 kwa lengo la kujenga jengo hilo ambazo ni fedha za Maendeleo Kwa Ustawi wa  Taifa na Mapambano dhidi ya Covid-19.

“Tumeridhika na ujenzi wa jengo hili, kilichobaki ni uwekaji wa samani katika jengo hili hivyo wizara iharakishe mchakato wa ununuzi wa samani ili wanachuo watakapofungua waweze kukitumia,” alisema.

Naye  Kaimu Mkuu wa ATC, Profesa Musa Chacha alisema mradi huo upo katika hatua za umaliziaji na ni wa madarasa nane yenye uwezo kuchukua wanafunzi 800 kwa wakati mmoja, maabara sita zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 270.

Pia kuna ofisi 26 zenye uwezo wa kuchukua watumishi 104 na kukamilika kwa jengo hilo kutahudumia  wanafunzi 1,025 na watumishi 104 kwa wakati mmoja ikiwemo kupunguza msongamano katika madarasa na maabara.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button