Kamati ya Kudumu ya Bunge yampigia chapuo Mkurugenzi NHC

WABUNGE ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wamesifu ubunifu na utendaji wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemiah Mchechu.

Walisema hayo Dodoma baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Mchechu kuwasilisha kazi zilizofanywa na NHC.

Mbunge wa Rorya, Jafari Wambura alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumrudisha Mchechu aongoze NHC.

Advertisement

Wambura alisema kabla ya kijana huyo kuondolewa kwenye uongozi wa shirika hilo alikuwa na maono kuhusu sekta ya nyumba hivyo ni wakati mwafaka kwake kuyatimiza kwa faida ya nchi.

“Mchechu ametoa taarifa nzuri iliyojibu maswali mengi ikiwemo ya mkwamo wa miradi mbalimbali ya NHC, lakini kwangu ninachokiona, siyo tu amejipanga kuanzia alipoishia ikiwemo kumalizia miradi ya Morocco square na Kawe 711, Mchechu amekuja na ubunifu mwingine wa kuongeza nyumba nyingine katika eneo unakotekelezwa mradi wa Kawe 711, hilo ni jambo kubwa sana,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha vijana, Asia Halamga alisema majibu ya Mchechu kwa kamati hiyo yaliondoa sintofahamu kwake hasa kuhusu miradi iliyokwama.

“Kitendo cha serikali kutoa ridhaa kwa NHC kukopa, hatimaye imalizie miradi hiyo tajwa, ni kiashiria kuwa serikali inaliamini shirika hilo kuwa litamalizia miradi hiyo pasi na shaka yoyote na nimalizie kwa kuipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Shirika lake la nyumba la Taifa (NHC) kwa kazi nzuri inayosababisha kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Halamga.

Katika kikao hicho Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema serikali itahakikisha NHC inatekeleza mpango kazi unaojumuisha kumalizia miradi iliyokwama ukiwemo wa Morocco square na Kawe 711.

Ridhiwani alisema katika kikao baina ya wizara na kamati hiyo ya bunge, ajenda zilikuwa mbili ikiwemo ya kueleza kazi zilizofanywa na NHC na Wizara kutoa taarifa ya mchakato wa uundwaji ama marekebisho ya sera ya ardhi ya mwaka 1999 umefikia wapi.

“Ili kuukamilisha mradi wa Morocco Square uliosimama toka 2018 kwa kukosa fedha, serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeridhia Shirika kukopa ili kukamilisha pia miradi mingine iliyokwama ukiwemo wa Kawe 711 na mpaka sasa Shirika limekopa kiasi cha shilingi bilioni 44.7 kwa ajili hiyo,” alisema.