KAMATI ya wataalamu wa ramani mgodini kutoka Chuo cha Madini Dodoma imetoa ripoti kwamba madini kilo nne yalichimbwa mita 650 ndani ya kitalu C kinachomilikiwa na serikali na mwekezaji mzawa, Onesmo Mbise.
Pia kamati hiyo imebaini kuwa mageti yaliyowekwa na kampuni ya Gem & Rock Venture inayochimba katika kitalu B yaliwekwa ndani ya mgodi katika kitalu C.
Ofisa Mfawidhi wa Wizara ya Madini mkoani Manyara, Mernad Msengi amesema kamati hiyo imeagiza kampuni ya Gem & Rock Venture kuwa mageti waliyoweka chini ya ardhi yazingatie leseni husika na madini yaliyozalishwa katika eneo la mgogoro yataendelea kushikiliwa na serikali.
Msengi alisema mgodi huo katika kitalu B utaendelea kusimamisha shughuli za uchimbaji hadi itakaporekebisha makosa yaliyoelekezwa na Wizara ya Madini kuhusu ukiukwaji wa leseni uliofanywa na kampuni ya Gem & Rock Venture.

Alisema timu hiyo ya wataalamu ilifanya kazi kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenye Wilaya ya Simanjiro, viongozi wa mgodi wa Kitalu C na B na baadhi ya maofisa wa Wizara ya Madini.
Viongozi wa kampuni ya Gem & Rock Venture katika mgodi kitalu B walituhumiwa kuchimba madini katika mgodi kwenye kitalu C kinachomilikiwa na serikali na mwekezaji.
Ilidaiwa kuwa wachimbaji 30 kutoka kampuni ya Gem & Rock Venture katika kitalu B walivamia kitalu C na kutoweka na madini ya tanzanite kilogramu nne lakini maofisa wa Wizara ya Madini Mirerani walifanikiwa kuyakamata na kuyahifadhi katika ofisi ya madini Mirerani.