DODOMA: WIZARA ya Ujenzi imesema mfumo wa kamera za CCTV na taarifa za vipimo vya uzito wa magari utafungwa katika mizani 56 ya kupimia magari. Imelieleza Bunge kuwa wizara hiyo kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) inaendelea na taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mshauri elekezi atakayefunga mfumo huo.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.
SOMA: Trafiki kuondolewa barabarani kukabili rushwa
“Hadi sasa mfumo wa aina hiyo umefungwa katika mizani 13, ambao unasaidia utendaji kazi wa uwazi na hivyo kupunguza au kuondoa mianya ya rushwa,” amesema Bashungwa.
Amesema mizani iliyofungwa mfumo huo ni; Vigwaza (Pwani), Mikumi, Mikese (Morogoro), Nala (Dodoma), Njuki (Singida), Mpemba (Songwe), Mingoyo (Lindi), Himo 2 (Kilimanjaro), Mutukula (Kagera), Usagara (Mwanza) na Makuyuni (Arusha).
Bashungwa alisema ili kuendelea kudhibiti uzito wa magari barabarani wizara kupitia Tanroads imejenga mizani mipya minane. Alitaja mizani hiyo ni Mikumi (Morogoro), Matundasi (Mbeya), Mdori (Manyara), Uvinza (Kigoma), Nyantare na Rubana (Mara), Igagala (Njombe) na Mingoyo (Lindi).
“Maandalizi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mizani ya Kizengi (Tabora) yanaendelea. Aidha, mizani ya Mikese North (Morogoro) na Uyole (Mbeya) imeboreshwa kutoka mizani inayopima uzito wa magari kwa ekseli moja na kuwa mizani inayopima uzito wa magari kwa kundi la ekseli,” amesema Bashungwa.
Alisema wizara hiyo kupitia Tanroads imefunga mizani ya kisasa yenye uwezo wa kupima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo. Alisema hadi kufikia Aprili 2024, wizara imefunga mizani mitano ya aina hiyo katika vituo vya mizani vitatu.
Vituo hivyo na idadi ya mizani kwenye mabano ni Mikese (1), Mikumi (2) na Rubana (2) hivyo kufikisha jumla ya mizani 20 inayopima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo.
Amesema pia wizara kupitia Tanroads imeunganisha mfumo wa upimaji uzito wa magari na mifumo mingine ya Mamlaka ya Mapato (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mfumo wa malipo ya Serikali (GePG) katika mizani ya mfano ya Kimokouwa iliyopo mkoani Arusha. Bashungwa alisema kuunganishwa kwa mfumo huo kutarahisisha wasafirishaji kupata moja kwa moja namba za malipo baada ya gari kubainika kuzidi uzito na hivyo kuondoa changamoto kwa wasafirishaji kutumia muda mrefu kwenye vituo vya mizani.