SERIKALI imepanga kuanza kampeni kabambe ya kitaifa ya kupambana na matumizi ya vifungashio kuwa vibebeo iliyolenga kuanza Jumatatu ijayo nchini kote.
Hatua hiyo ni katika kutekeleza agizo la Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyeagiza mikoa yote kukabiliana na matumizi yaNa Anastazia Anyimike, Dodoma
Agizo hilo limetolewa Ijumaa jijini hapa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo wakati wataalamu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) walipokutana kujadili utekelezaji wa sheria ya mazingira.
Dk Jafo alisema tangu serikali izuie matumizi ya mifuko ya plastiki, kumekuwa na mafanikio makubwa ingawa sasa kumekuwa na changamoto ya watu kutumia vifungashio kuwa vibebeo.
“Katika utunzaji wa mazingira dunia ilikumbana na changamoto kubwa sana ya mifuko ya plastiki na kutokana na changamoto hiyo, tukiwa na mkakati mkubwa wa kuja na Kanuni ya Sita ya Mwaka 2019 kwa lengo la kutokomeza mifuko ya plastiki.
“Hata hivyo, sheria ilitoa unafuu kwa kuruhusu vifungashio ili kuwasaidia wajasiriamali wadogo ambao wanafunga karanga, ubuyu na tambi, lakini imejitokeza changamoto kwa baadhi ya watu wasio waaminifu wamegeuza vifungashio kuwa vibebeo, jambo hili limekuwa changamoto kubwa,” alisema Dk Jafo.
Kutokana na hali hiyo, aliagiza ifanyike oparesheni kabambe ya kuhakikisha mifuko ya plastiki haionekani tena katika mitaa.
Katika kutekeleza hilo kwa ufanisi, NEMC imetakiwa kushirikiana na mamlaka za serikali za mitaa na sekretarieti za mikoa katika kila kanda ya baraza hilo.
Dk Jafo alisisitiza oparesheni hiyo iguse masoko, magulio, madukani na bucha za samaki na nyama.
Alisema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan amezindua filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ ambayo imeongeza watalii na kusema ni vyema kuunga mkono juhudi hizo kwa kuweka miji katika hali ya usafi.
Aidha, ametoa miezi miwili kwa Mkurugenzi wa Mazingira na Kitengo cha Sheria cha wizara hiyo kufanya mapitio ya sheria ili kuona namna ya kuboresha kanuni ili kubana zaidi matumizi ya vifungashio kuwa vibebeo.