OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ofisi za Wakuu wa Wilaya mkoani humo na wadau mbalimbali wa afya wameandaa kampeni ya kupima afya bure kwa wananchi wa Dar es Salaam itakayodumu kwa siku 10.
Akizungunza leo Julai 5, 2023, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema kampeni hiyo itaanza Julai 10 hadi 19 , 2023 na kuhusisha wilaya zote za Dar es Salaam, lengo kuu likiwa ni kusaidia wakazi wa mkoa huo kujua hali ya afya zao bila gharama yoyote.
Chalamila amesema uzinduzi rasmi wa kampeni hiyo utafanyika viwanja vya Zakhiem Mbagala Julai 10 na kisha kuendelea katika Wilaya zote tano na wanakusudia kuwafikia wananchi zaidi ya 20,000.
“Wananchi watumie fursa hii ambayo pia Rais Samia anasisitiza kupima afya ili kujua hali zao kiafya, tunalenga kuwafikia wakazi zaidi ya 20,000 wa Dar es Salaam, walengwa haswa ni wakazi wa Dar es Salaam, lakini tunawakaribisha pia na wakazi wa mikoa ya karibu,” amesema Chalamila.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Julius Mwaiselage amesema kuna ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kwa jinsi zote, hivyo wananchi wanapaswa kuitumia vyema fursa hiyo kujua hali zao za kiafya.
” Magonjwa yasiyoambukiza mfano saratani yanaenea kwa kasi sana, hasa saratani ya mlango wa kizazi, saratani ya matiti, tezi dume na saratani ya ngozi na watu wanaugua magonjwa haya bila kujijua hivyo ni vyema wakatumia nafasi kuja kupima,” amesema Dk. Mwaiselage.
Mratibu wa Kampeni ya Afya Check, Dk. Isaac Maro amesema zaidi ya asilimia 75 ya magonjwa yasiyoambukiza yanasababishwa na mtindo wa maisha na mara nyingi watu hawajijui kama wameathirika hivyo ni vyema kupima afya kila wakati.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Rashid Mfaume amesema kuna sababu nyingi zinazofanya watu kushindwa kupima afya zao, hasa gharama hivyo wameona kilio cha wananchi na ndio sababu ya kampeni hiyo na amewahakikishia wananchi uwepo wa madaktari bingwa kwenye kampeni hiyo.