Kampeni ulaji sahihi yatua Nyanda za Juu

MIKOA sita ya Nyanda za Juu Kusini imeanza kupata mafunzo ya mwongozo wa ulaji sahihi wa chakula hatua inayolenga kukabiliana na changamoto ya udumavu katika kanda hiyo.

Mafunzo hayo ambayo hatua yake ya awali inahusisha maafisa lishe wa mikoa hiyo ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Songwe na Katavi yanafanyika kwa siku nne mjini Iringa.

Akifungua mafunzo hayo, Ofisa Kilimo Mkuu na Mratibu wa masuala ya lishe wa Wizara ya Kilimo, Magret Natai alisema mafunzo hayo yatawawezesha maofisa lishe kuutumia mwongozo huo kuihamasisha jamii juu ya ulaji unaofaa.

Natai alisema mwongozo huo unayataka makundi yote katika jamii kama wajawazito, watoto, wazee na watu wa rika zote kutambua jinsi ya kuandaa pamoja na namna sahihi ya ulaji chakula, ili kuimarisha afya ya mwili na kuongeza kinga dhidi maradhi mbalimbali ukiwemo udumavu.

“Baada ya mafunzo haya ni matarajio yetu jamii nzima ya mikoa hii na Tanzania kwa ujumla kwa kupitia maofisa lishe hawa ambao ndio watekelezaji wa mradi itaanza kuelewa juu ya uandaaji sahihi wa chakula pamoja na ulaji unaofaa,” alisema.

Ofisa Lishe wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na Chakula na Kilimo (FAO) nchini, Stella Kimambo alisema watatumia usafiri wa daladala, programu za mapishi na utafiti utakaofanywa nyanda za juu kusini juu ya usalama wa chakula kama sehemu ya mikakati ya kufikisha elimu kwa jamii.

Kimambo alisema mpaka sasa tayari shule 100 za nyanda za juu kusini zinatekeleza programu za kilimo lishe kupitia bustani, huku shule 10 za mkoani Njombe zikitekeleza programu za chakula.

Naye Siatu Mbwambo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), alisema jamii ya mikoa ya nyanda za juu kusini inapitia changamoto kwenye masuala ya ulaji na kuwaagiza maofisa lishe waliohudhuria mafunzo hayo kutumia mafunzo watakayopata, ili kufikia lengo la kampeni ya kitaifa ya lishe bora ni mtaji.

Akitoa maoni yake juu ya mafunzo hayo, Ofisa Lishe wa Manispaa ya Songea, Albert Christopher alisema jukumu lao ni kurudi kwenye jamii kwa ajili ya kuwaelimisha jinsi ya kuandaa chakula na namna sahihi ya ulaji.

Pamoja na kwamba mikoa ya nyanda za juu kusini inaongoza kwa uzalishaji wa chakula alisema baadhi ya watu wake hawazingatii namna bora ya uandaaji pamoja na ulaji sahihi wa chakula hali inayowafanya wawe na changamoto mbalimbali za kiafya.

Habari Zifananazo

Back to top button