Kampeni ya Ebola yafika patamu

Sasa ni mtaa kwa mtaa hadi 'gest house '

KAMPENI za kujikinga na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mkoani Kagera zimeingia katika hatua nyingine baada ya Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kuanza kupita nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu, mtaa kwa mtaa, nyumba za kulala wageni  kwa lengo la kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa na hauingii nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma, Dk Ama Kasangala amekuwa akitembea kwa miguu mitaani, masokoni na nyumba za kulala wageni kuhakikisha elimu ya namna ya kujikinga na Ebola inawafikia wengi.

Akizungumza leo Septemba 9, 2022 katika soko la Bunazi lililopo Wilaya ya Misenyi, Dk Ama amesema kampeni ya mtu kwa mtu anayoifanya ina ushawishi mkubwa kwa vile inamfikia hata asiyehudhuria mikutano ya kampeni za kudhibiti ebola inayofanywa kuanzia ngazi za chini za mitaa na vijiji.

“ Tutaendelea na kasi hii, tutashambulia kila mahali, nyumba za wageni chumba kwa chumba, wageni wanaingia na kutoka wapate elimu ya kujikinga na ebolà na tutashambulia mitaani na tutashambulia nyumba hadi nyumba na mtu hadi mtu, hakuna kulala, serikali haitalala hadi hapo nchi jirani itakapotuhakikishia wameudhibiti ugoñjwa huu,” amesema

Amesema, tayari wametoa maagizo kwenye nyumba zote za wageni kuzingatia afua za afya kwa kuweka sabuni, maji tiririka na kuwapima joto wageni wote wanaoingia.

“Tumewaelimisha na kama kuna mgeni muhisiwa basi wapige simu namba 199 ni bure na kutoa taarifa na wataalamu wetu watachukua hatua kwa haraka.

Amesema mbali na kutembea nyumba hadi nyumba, lakini bado wataendelea kutumia magari ya matangazo kuzunguka kwenye maeneo ya pembezoñi kuelimisha wananchi.

Aidha, kātika kampeni hizo Dk Ama amegawa vipeperushi vyenye ujumbe mbali mbali za dalili za ugonjwa wa Ebola na namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Katika soko la Bunazi, Dk Ama amegawa vizibao vyenye ujumbe wa kujikinga na Ebola kwa madereva wa bodaboda, amegawa vipeperushi kwa wafanyabiashara mbali mbali na wananchi waliofika kununua mahitaji ikiwemo flashi ambazo zinazungumzia ugonjwa huo wa Ebola.

Dk Ama amesema serikali imeweka nguvu kubwa mkoani Kagera kutokana na mkoa huo kuingiliana kwa karibu na Uganda.

Habari Zifananazo

Back to top button