Kampeni ya upandaji miti kuanza kesho Mtwara

Bodi ya Maji  Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini kesho inatarajia kuzindua kampeni  ya upandaji miti rafiki katika chanzo cha maji kilichopo Mtawanya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Hatua hiyo ni katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu kwenye vyanzo vya maji.

Akizungumza leo mkoani humo, Mkurugenzi wa Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini, Jumanne Sudi amesema kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya Wananchi kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii katika vyanzo vya maji ikiwemo kilimo, kuchoma mkaa, uchimbaji wa madini pamoja na utupaji wa taka sumu.

Advertisement

‘’Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya Wananchi kuendesha shughuli za Kijamii kwenye vyanzo vya maji  kama vile kilimo, kuchoma mkaa, uchimbaji wa Madini pamoja na utupaji wa taka sumu’’,amesema Sudi

Amesema, kutokana na shughuli hizo ambazo zimekuwa zikufanywa na Jamii katika vyanzo hivyo  vya maji kwa kiasi kikubwa zimekuwa  zikileta athari katika vyanzo hivyo ikiwemo uwepo wa mabiliko ya tabia Nchi, vyanzo kushindwa kuzalisha maji vizuri.

Kutokana na uwepo wa changamoto hizo ni vema Jamii  ikaacha kufanya hivyo na badala yake kujitokeza kupanda miti rafiki wa maji katika vyanzo vya maji ili kuvifanya vyanzo hivyo kuwa salama wakati wote.

Kampeni hiyo ya upandaji miti itazinduliwa na Mkuu wa  Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abas katika chanzo cha maji kilichopo Mtawanya Manispaa ya Mtwara Mikindani Mkoani Mtwara kwa kushirikiana na Wananchi wanaoishi katika eneo hilo.