ZAIDI ya kampuni 250 zinatarajia kushiriki Kongamano la Suluhu za Mazingira (NBS) linalolenga kujadili fursa za uwekezaji katika soko la kaboni na kuongeza uelewa kwa wadau ikiwa ni hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza kuhusu tukio hilo leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Operesheni wa Chama cha Maendeleo ya Maeneo Tengefu (ADAP), Yves Hausser amesema mkutano huo utavutia washiriki kutoka Tanzania na nje ya nchi na utafanyika Novemba 16,2023.
Ameongeza kuwa mkutano wa NBS umekuja wakati muwafaka kwani utasaidia pia kutatua changamoto za uharibifu wa mazingira na jinsi ya kupunguza hewa ukaa duniani.
“Tumegundua kuwa Tanzania kuna shauku kubwa ya mikopo ya kaboni lakini kwa kweli kuna watu wachache wanaoelewa jinsi mchakato unavyofanya kazi na tunahitaji wadau nchini kuelewa vyema mfumo wa mikopo ya kaboni.” amesisitiza.
Aidha amebainisha kuwa mkutano huo ni hatua ya kwanza katika kuongeza uelewa na kuwafanya wadau kuuelewa vizuri mfumo huo.
Amewahimiza wadau hao ikiwemo serikali kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuongeza uelewa juu ya mikopo ya kaboni ili kuwavutia watu wengi zaidi kushiriki katika shughuli hizo na hatimaye kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyopo duniani.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Kaboni Afrika (ACA) Cosmas Tungaraza amesema mkutano huo unalenga pia kuwafahamisha wadau wakuu, serikalini na sekta binafsi juu ya uwezo, lakini pia masharti, ya kuendeleza soko la kaboni, na kwa ujumla zaidi uthibitisho wa athari.
Ametaja idadi ya mada zitakazojadiliwa ni jinsi ya kuendeleza miradi ya kaboni kwa jamii kwa ufanisi, ushirikiano kati ya wadau mbalimbali,jinsi fedha zinazopatikana zinavyotumika katika ngazi ya jamii na jinsi zinavyochangia maendeleo.
Amebainisha kuwa mada nyingine ambayo itajadiliwa ni mfumo wa kisheria wa Bbashara ya Kaboni Tanzania,serikali zinatumiaje usimamizi wa maliasili katika masoko ya kaboni na kwa nini uwekeze katika Sekta ya kaboni ya Tanzania?
.
“Wazo ni kukuza hali ya hewa inayofaa kwa mabadiliko katika kiwango cha uwekezaji huu, ili uwezo kamili wa sekta hii uweze kupatikana.
Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Kaboni Tanzania ,Azalia Kilimba amesema wameazisha miradi ya soko la kaboni katika ukanda wa kaskazini ambayo imekuwa na manufaa kwa jamii hiyo.
“Tumenzisha miradi huku Karatu, Mbulu, Kiteto, Tanganyika, Tunduru na Namtumbo na wanufaika wa kwanza ni Wananchi ambao wapo karibu na miradi na miongoni mwa manufaa wanazopata ni huduma za kijamii na pia watu wanaoajiriwa wanatoka ndani ya jamii husika,”ameeleza.
Amesema mkutano huo utatoa fursa pana ya kuongeza uelewa na kukuza soko la kaboni pamoja na uhifadhi wa mazingira nchini.
Mkutano huo umeandaliwa na kamati inayoundwa na wafanyakazi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Maliasili na Utalii, wakala wa Africa Carbon, ADAP, AxessImpact, Carbon Tanzania, National carbon Monitoring Center na ADIS.