Kampuni yaipa sekondari mifuko 153 ya saruji
KATIKA kuunga mkono juhudi za serikali, Kampuni ya Bima ya Sanlam imechangia ujenzi wa shule ya sekondari katika Kijiji cha Mayamaya mifuko 153 ya saruji.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mifuko ya saruji yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 2.7, Meneja Maendeleo ya Biashara wa Kanda ya Kati wa kampuni hiyo, Said Makongwa alisema hatua hiyo ni katika kuthamini juhudi na kazi bora inayofanywa na serikali katika kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa elimu.
“Tumeamua kuunga mkono juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya elimu kwa kutoa mchango wa mifuko na saruji 153 kufanikisha ujenzi wa shule ya sekondari inayojengwa Kijiji cha Mayamaya kilichopo Wilaya ya Bahi, Mkoa wa Dodoma,” alisema na kuongeza:
“Kampuni yetu inajisikia fahari kuwa ya kwanza kuitikia wito wa Serikali ya Wilaya kuja kutoa msaada huu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari.”
“Sisi tumeguswa na wanafunzi wanaosafiri umbali mrefu kwenda vijiji vingine kwa ajili ya kupata elimu ya sekondari. Tunaamini uwepo wa sekondari hapa utaboresha upatikanaji wa elimu na utaleta chachu ya maendeleo katika kijiji hiki.”
Alisema pia wanaamini kuwa upatikanaji wa elimu karibu utawapa muda wa kutosha wa wanafunzi wa kujisomea na kuongeza ufaulu katika mitihani hususani kwa watoto wa kike.
Kampuni ya Bima, Sanlam yenye matawi Pemba, Mbeya, Arusha, Mbagala, Zanzibar, Dodoma na Mwanza ni kampuni bobezi na bingwa katika utoaji wa huduma za bima za maisha, vyombo vya moto, majengo, vikundi wakandarasi, biashara na nyinginezo.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mwenyekiti wa Kijiji, Jonathan Chibalangu aliishukuru kampuni hiyo kwa kuitikia ombi na kusaidia ujenzi wa shule hiyo ambao umeanza kwa nguvu za wananchi.
“Tunawashukuru kwa kuunga mkono juhudi za wananchi walioamua kuanza kujega shule ya sekondari ili kuwapunguzia watoto wao adha ya kutembea umbali mrefu,” alisema.
Chibalangu pia aliomba kampuni na taasisi mbalimbali kuendelea kuisaidia serikali ya kijiji kuwa na sekondari na kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi inajumuisha madarasa manne, ofisi ya walimu na vyoo.
Kaimu Mwenyekiti wa tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kijiji cha Mayamaya, Emmanuel Mkochechi alipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono serikali ya CCM ambayo imejipambanua katika kuhakikisha hakuna mtoto wa Kitanzania anakosa fursa ya kupata elimu.
Naye dada mkuu wa Shule ya Msingi Mayamaya, Nadhifa Harifa alisema ujenzi wa shule hiyo utawapa motisha wale walio shule ya msingi kusoma kwa bidii wakiwa na uhakika wa kuendelea na elimu ya sekondari eneo la karibu.