Kampuni yaiunga mkono Serikali maboresho elimu

KAMPUNI ya ukandarasi ya Kalpataru Power Transmission Limited inayoshughulika na umeme imetoa ufadhili na kujenga jengo la utawala la kisasa kwa ajili ya matumizi ya ofisi za walimu wa shule ya Msingi Azimio iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Jengo hilo linagharimu Sh milioni 100. Litasaidia walimu 48 waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya muda mrefu ya kukaa katika mavaranda ya madarasa na nje chini ya vivuli vya kutokana na uhaba wa majengo kwenye shule .
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa ni shule shikizi na baadaye kuwa shule kamili iliyosajiliwa. Jengo hilo la kisasa lina ofisi ya mwalimu mkuu , mhasibu , chumba maalumu cha kutokea ushauri nasaha kwa wanafunzi pamoja na ofisi mbili za walimu.
Ufadhili huo umechangiwa kwa asilimia 100 na meneja wa mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa Reli ya Mwendokasi (SGR) wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Rosamystica Lutenganya anayesimamia kipande cha Morogoro- Dodoma.
Mhandisi Lutenganya amesema hayo wakati wa makabidhiano kwa uongozi wa Manispaa ya kwamba kabla ya kupatikana kwa ufadhili huo na kujengwa kwa jengo hilo aliguswa kuwaona walimu kikaa nje na chini ya vivuli vya miti zikiwa ni ofisi zao .
“Wakati ninawajibika kusimamia ujenzi wa line ya umeme ya Morogoro- Dodoma ya matumizi ya reli ya SGR ,kila nikipitia niliwaona walimu wapo nje na kwenye miti zikiwa ni ofisi zao na wengi wao ni wanawake ,hili lilinigusa na kupata wazo la kuisaidia shule hii ipate jengo la utawala “ anasema Mhandisi Lutenganya
Amesema Kampuni ya Kalpataru ya nchini India iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa njia hiyo inao utaratibu wa kusaidia vitu mbalimbali kwenye jamii .
Alisema baada ya kuona changamoto walizokuwa wakizipata walimu wa shule hiyo aliwasilisha wazo lake kwa uongozi wa shule hiyo na kwa idara ya elimu kwa kuandika andiko la kuomba ufadhili kutoka kwa kampuni hiyo ili kujengewa jengo la utawala.
Mhandisi Lutenganya alisema baada ya kuandika andiko na michoro ya ramani na makadirio ya fedha kiasi cha Sh milioni 100 na kuwasilisha kwa Menenimeti ya Kampuni ambayo iliridhia maombi hayo na kutoa fedha hizo zilizotumika kujenga jengo hilo ulionza Septemba 2022 na kukamilika Februari 2023.
Makamu wa Rais Kampuni hiyo ,Saroj Kumar Sahoo kwa niaba ya menejimenti ya Kampuni hiyo amesema baada ya kupitia andiko la kuomba ufadhili wa kujengewa jengo hilo , uongozi wa kampuni uliridhia kutokana na uhalisia wake na kutoa ufadhili wa takribani sh milioni 100.
Sahoo amesema kupitia jengo hilo amewaomba walimu kulitumia vizuri na kulitunza ili kuwezesha watoto wapatie elimu nzuri kwa ajili ya maisha yao ya baadae.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo ,ufadhili uliotolewa ni kwa mara ya kwanza tangu imeanza kazi hapa nchini baada ya kukupokea ombi na andiko hilo.