KAMPUNI ya Alliance One Tobacco Tanzania Limited (AOTTL), imesema hadi sasa imewalipa wakulima wa tumbaku Dola za Marekani milioni 71.9 (takribani Sh bilioni 179.8) katika msimu huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa AOTTL, Ephraim Mapoore alisema fedha hizo zilitumika kulipa wakulima zaidi ya 12,000 walioingia mkataba msimu huu baada ya kuwasilisha tumbaku yao yenye ubora wa juu kwa kampuni hiyo.
Alibainisha kwamba malipo yalifanyika kwa kuzingatia agizo la serikali la hivi karibuni kuhusu malipo kufanyika ndani ya kipindi ambacho wakulima wanapaswa kupokea malipo yao,” alisema.
Hivi karibuni, serikali iliagiza malipo yote ya tumbaku kwa wakulima yafanywe ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya kukamilika kwa soko na kwamba malipo yote lazima yakamilishwe kwa Dola ya Marekani.
“Wakati sheria zinazoongoza zinawataka wanunuzi wote wa tumbaku kulipia tumbaku iliyonunuliwa ndani ya siku 14, sisi kama AOTTL tumefanikiwa kuwalipa wakulima wetu walioingia mkataba ndani ya siku nne,” alisema Mapoore.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB), Stanley Mnozya alisema malipo ya wakulima wa tumbaku kwenye maeneo mbalimbali yalichelewa kutokana na changamoto ya uhaba wa Dola za Marekani na uzalishaji wa tumbaku kwa kiwango cha juu kuliko uwezo wa soko.