Kampuni yapewa siku 7 maji yasambae Msomera
WIZARA ya Maji imetoa siku saba kwa Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Handeni, Hosea Joseph amsimamie mkandarasi wa kampuni inayotekeleza Mradi wa Maji katika Kijiji cha Msomera ahakikishe maji yanafi ka kwenye tangi na kuyasambaza kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi alitoa agizo hilo jana alipokagua mradi wa maji kijijini hapo katika Kata ya Misima.
“Niwapongeze Ruwasa ambao wanasimamiwa na Mhandisi Upendo Omari ambaye anafanya kazi nzuri sana hapa tulipo kuna tenki kubwa ambalo lililetwa kutoka nje lengo kuhakikisha jamii ya Msomera inapata maji toshelevu na kwa kupata tenki hili visima vilivyochimbwa hapa vinakwenda kutumika vizuri,” alisema Mahundi.
Alisema kuna kisima ambacho kinatoa maji mengi na wanategemea ndani ya wiki moja kutoka jana kitaanza kusafirisha maji kutoka hapo kwenda kwenye tangi na baadae usambazaji wa maji kwa wananchi watakaohamia Msomera wanapata huduma ya maji.
Mahundi alisema wamejenga maeneo matatu ya kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Msomera ili wafugaji wapate maji ya kutosha na kuna mikakati ya kilimo cha umwagiliaji itakayotolewa na Wizara ya Kilimo.
Alisema maji yakishafika kwenye tangi yatakwenda kwenye usambazaji wa vichotea maji na kwa wananchi watakaokuwa na uhitaji wa kuyavuta kwenye majumba yao, watapewa vigezo na masharti nafuu ili wavute maji.
Naibu Waziri alisema serikali imedhamiria kumtua mama ndoo kichwani ili wafanye shughuli nyingine za kuchangia Pato la Taifa. Meneja wa Ruwasa Mkoa wa Tanga, Upendo Omari alisema watahakikisha ndani ya siku tatu wananchi hao wanapata maji.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Handeni, Hosea Joseph alisema watamsimamia mkandarasi Mponela Construction and Co. Ltd atekeleze ujenzi wa mradi wa maji kijijini hapo.