MKUU wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amesema wamejipanga kufuatilia, kuchunguza na kuzichukulia hatua kampuni binafsi zinazotoa huduma ya ulinzi wilayani hapa kwa kutumia mgambo ambao hawajapitia mafunzo ya Jeshi la Akiba.
Alisema hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku chache baada ya kutokea kwa uvamizi wa kituo cha mafuta katika Kata ya Bukoli wilayani hapa ambapo walinzi waliokuwa eneo la tukio walishindwa kudhibiti wahalifu.
Shimo alisema hayo juzi alipokuwa akizungumzia hali ya ulinzi na usalama ya wilaya katika kikao cha nne cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhitimisha mwaka wa fedha 2021/2022.
“Tulichokiona kwenye uvamizi pale kwenye kituo cha mafuta cha Bukoli, kwanza walinzi wale waliokuwa zamu mmoja hakuwa na mafunzo ya Jeshi la Akiba, walivyokutwa na kuvamiwa ni dhahiri kwamba mafunzo ya jeshi la akiba ni muhimu sana,” alisema.
Aliongeza: “Tunafuatilia kwa ukaribu kujua ni kwa nini kampuni hizi binafsi zinaajiri watu ambao hawana mafunzo, kwa sababu hata baada ya kuvamiwa, tulipoomba ulinzi mwingine kutoka kampuni ileile tukaletewa mlinzi ambaye hana mafunzo tena,” alisema.
Alisema kampuni za ulinzi kuajiri walinzi wasio na vigezo vya mafunzo ya jeshi la akiba haiimarishi ulinzi bali inadhoofisha hali ya ulinzi na usalama na kusababisha ongezeko la matukio ya uhalifu kwenye maeneo mbalimbali wilayani hapa.
Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Geita, Jeremiah Mahinya alisema tayari Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeanza kupokea vijana kwa ajili ya mafunzo ya jeshi la akiba na hivyo ni fursa kwa wananchi na vijana kujiunga wakidhi vigezo vya ulinzi.