Kampuni za ununuzi wa mbegu za pamba lawamani

SERIKALI wilayani Geita imesikitishwa na kampuni za ununuzi wa mbegu za pamba kushindwa kutekeleza maazimio waliyokubalina ikiwemo kuanzisha mashamba darasa.

Katibu Tawala wa wilaya ya Geita, Thomas Dimme alieleza hayo juzi katika kikao cha tathimini ya msimu wa kilimo 2022/23 pamoja na maandalizi ya msimu wa kilimo ujao wa 2023/24.

Alisema azimio kuu la kikao cha tathimini kilichopita kilielekeza kampuni zinazonunua mbegu za pamba yashirikiane na Vyama vya Ushirika (Amcos) kulima mashamba darasa.

Alisema lengo na dhamira ya kuanzisha mashamba darasa ni kutoa mwanga kwa wakulima juu ya njia sahihi za kilimo cha pamba na kurejesha uhai wa zao hilo la biashara.

Alisema inashangaza kuona mbali na maazimio hayo lakini mpaka sasa msimu wa kilimo ukiwa unaelekea mwisho hakuna kampuni wala Amcos imeweza kulima shamba la mfano.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe aliwataka wakulima kuachana na kilimo cha mazoea kutokana na mabadiliko ya tabianchi badala yake wazingatie ushauri wa wataalamu.

Awali, Kaimu Ofisa Kilimo, Wilaya ya Geita Richard Kapyera alisema serikali inaendelea na juhudi za kufufua kilimo cha zao la pamba kupitia usambazaji wa pembejeo ikiwamo mbegu na viuadudu.

“Kwa mwaka 2021/22 tulikuwa na tani 334,680, kwa mwaka 2022/23 tuna tani 450,000 za mbegu bora, lakini pia 2021/22 tulikuwa na kilo 227,200 za viuadudu lakini msimu huu tuna viuadudu kilo 341,244,” alisema.

“Kwa msimu uliopita, hatukuwa na vinyunyizi, kwa msimu huu tumepokea vinyunyizi 900 na pia tumepata majembe 10 ya kisasa, majembe manne halmashauri ya mji na sita halmashauri ya wilaya,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button