Kamwe: Tutachukua hatua kunyimwa goli jana

AFRIKA KUSINI: Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe amesema uongozi wa timu hiyo utachukua hatua juu ya tukio la utata lililotokea jana kwenye mchezo wa mkondo wa pili robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Katika mchezo huo uliomalizika bila kufungana katika dakika 90, mpira uliopigwa na Stephan Aziz Ki umekuwa gumzo ambapo wengi wanaamini mpira huo ulivuka mstari na kupaswa kuwa goli lakini mwamuzi aliamua tofauti.

Amesema suala hilo tayari linafanyiwa kazi na watawasilisha rasmi pingamizi yao kunako Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwani wanaamini walikuwa na nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Hata hivyo licha ya kutolewa, Kamwe amewasifu wachezaji wa timu hiyo kwa namna walivyojituma katika michezo yote miwili ya robo fainali huku akikiri walikutana na moja ya timu bora barani Afrika.

Kamwe amewataka Wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho timu yao inaendelea na michuano mingine.

Habari Zifananazo

Back to top button