MRADI wa umeme wa Tanzania na Kenya unatarajia kuboresha huduma ya umeme mikoa ya Kanda ya Kaskazini
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa, mradi wa kimkakati wa umeme utakaounganisha Tanzania na Kenya kupitia kituo cha kupokea na kusambaza umeme cha Lemugur kilichopo mkoani Arusha, pia utaboresha huduma ya umeme katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Mramba ameyasema hayo mkoani Arusha, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha Lemugur mkoani humo, ambacho kitakuwa na uwezo wa kupokea na kusambaza umeme wa msongo mkubwa wa Kilovolti 400, kutoka Singida, Namanga hadi nchini Kenya.
“Mradi huu ni Mkubwa kwa nchi yetu, ni mradi wa kimkakati katika kuboresha huduma ya umeme nchini, pia kituo hiki cha Lemugur, kitaiunganisha Tanzania na Kenya kwenye umeme, na kitaboresha upatikanaji wa huduma ya umeme unaoikabili mikoa ya Kanda ya Kaskazini”, amesema Mhandisi Mramba.
Amesema, kituo cha Lemugur ni muhimu kwa serikali kwa kuwa, kinaunganisha njia ya umeme kutoka Tanzania kwenda Kenya kama ilivyo katika mpango wa serikali wa kutaka kuunganisha Tanzania na nchi nyingine kwa njia ya msongo mkubwa wa Kilovolti 400.
Pia, kituo hicho kitakuwa na uwezo kupeleka na kuboresha huduma ya umeme katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikiwemo Tanga, Arusha na Kilimanjaro.
“Kwa miezi kadhaa sasa, Mkoa wa Tanga umekuwa na changamoto za upatikanaji wa huduma ya umeme kwa kuwa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi mkoani humo imezidiwa uwezo kutokana na kuongezeka kwa mahitaji kutokana na uwepo wa viwanda vingi.; … “Hivyo kituo hiki cha Lemugur kitafanya mkoa wa Tanga kupata umeme kutoka vituo viwili ambapo kituo kingine ni Chalinze.”Amesema
Aidha, amesema kituo hicho pia kitakuwa na uwezo wa kusambaza umeme wa Msongo wa Kilovolti 33 katika Mkoa wa Arusha wenye shughuli nyingi za kiuchumi na utalii.
Amesema, serikali ina mpango wa kujenga njia nyingine ya kusafirisha umeme kwa kuunganisha nchi ya Zambia na Tanzania na kisha Uganda na Tanzania.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Mramba alitoa maagizo kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuwa kazi ya ujenzi katika kituo hicho ifanyike kwa ubora na viwango vinavyotakiwa na hadi kufikia Julai 31, 2023, ujenzi wa kituo hicho uwe umekamilika.
Aidha, ameagiza kuwa, mwezi Septemba mwaka huu, njia za kusafirisha umeme kutoka Arusha kwenda Tanga ziwe zimekamilika ili mkoa huo uwe na uwezo wa kupata umeme kutoka Mkoa wa Arusha.
Kwa upande wake, Mkandarasi anayetekeza mradi huo, Clive Sihwa kutoka Kampuni ya GOPA alimhakikishia Katibu Mkuu kuwa mradi huo utakamilika kwa wakati uliopangwa kwa kuwa sehemu kubwa ya ujenzi katika mradi huo imekamilika.
Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Mramba na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo walikagua njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa Kilovolti 400 katika eneo itakapojengwa Makao Makuu ya Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na Watu, mkoani Arusha.