Kanisa Katoliki lapongeza ujenzi bomba la mafuta

Kanisa Katoliki lapongeza ujenzi bomba la mafuta

BARAZA la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) limeridhishwa na mchakato wa ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka nchini Uganda hadi mkoani Tanga.

Katibu Mkuu wa TEC, Padri Dk Charles Kitima, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thadaeus Ruwa’ichi na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala wamesema Kanisa Katoliki nchini linaunga mkono utekelezaji wa mradi huo.

Walisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa mkutano baina ya TEC na wataalamu wa mradi wa EACOP.

Advertisement

Padri Kitima alisema mradi huo ni muhimu na Kanisa Katoliki linaridhishwa na mradi wa EACOP kwa kuwa unatekelezwa kwa tahadhari za kisayansi na akahimiza Watanzania wauunge mkono.

“Maaskofu wanaridhika kwa kuwa wanaona tahadhari zimechukuliwa na sheria za nchi na kimataifa kuhusu haki za binadamu zimezingatiwa…kanisa linapoona sheria za nchi na haki za binadamu zimezingatiwa na kulindwa, linaunga mkono maana kupitia mradi huu pia nchi itapata mafao na utajiri endelevu,” alisema.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema anaamini taasisi na nchi zinazopinga kutekelezwa kwa mradi huo wana sababu zinazohusu maslahi yao.

“Naamini huu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki utatekelezwa kwa uangalifu mkubwa wa usalama wa mazingira na maslahi mapana ya nchi zote husika yaani Uganda na Tanzania,” alisema na kuongeza:

“Nina wasiwasi na sababu zinazotolewa na baadhi ya watu, taasisi na nchi kupinga EACOP maana si za msingi na naona hao wana maslahi na sababu zao binafsi.”

Askofu Kassala alisema katika Mkoa wa Geita lilipo Jimbo la Geita, utekelezaji wa mradi huo pia utasaidia kurudisha uhifadhi wa mazingira yaliyoharibiwa.

“Tunafurahishwa na hatua ya EACOP kusisitiza utengenezaji wa mazingira bora ya watu kuishi, badala tu ya kuwapa fidia ya pesa ambazo watu wengine huzitumia kununua gari, likaharibika kisha wakaishi katika maisha ya uchungu na kuanza kulalamika,” alisema.

Meneja Mkuu wa EACOP, Tawi la Tanzania, Wendy Brown aliwaeleza maaskofu hao jana kuwa miongoni mwa mambo yaliyopewa kipaumbele katika utekelezaji wa EACOP ni teknolojia itakayopunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa.