VIONGOZI wa dini wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), wamewataka Wakristo na Watanzania kwa ujumla kuacha usaliti na matendo ya mmomonyoko wa maadili kwa taifa lao na badala yake waoneshe moyo wa huruma kama alivyoonesha Mwokozi wao Yesu Kristo wakati akiteswa msalabani.
Kauli hiyo imetolewa kwenye maeneo tofauti ya nyumba za ibada jana nchini wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu kukumbuka mateso ya Yesu Kristo msalabani, ambapo ibada ya Kitaifa ilifanyika katika Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi-Tunduru mkoani Ruvuma.
Akiongoza Ibada ya Ijumaa Kuu katika Kanisa la Azania Front mkoani Dar es Salaam, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliwataka Wakristo na Watanzania kwa ujumla kuacha usaliti.
Askofu Malasusa alisema badala ya kuwa wasaliti ni vyema wakatumikia nafasi walizopewa kwa weledi na maadili na wale walioamua kusaliti viongozi wao wanastahili kuombewa ili Mungu aondoe roho wa usaliti katika nafsi zao na hatimaye wawe watu wema na kutumikia jamii.
Akitoa mahubiri Askofu Dk Malasusa aliwataka Wakristo na Watanzania waoneshe moyo wa huruma na kusema jambo hilo litachangia taifa kupata watu wenye huruma hadi katika familia na watatunza pia rasilimali za taifa.
Alisema baadhi ya watu wakiwa kanisani wanaonesha huruma kwa Yesu Kristo lakini wakitoka nje hawana huruma na wanaangamiza taifa kwa usaliti kama alivyothibitisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Juzi nimesikia kwamba katika taifa letu mkaguzi amepita akaona watu waliopewa madaraka wanavyoyatumia vibaya. Mahali pa tano inakuwa tisa, pa tisa inakuwa 19 hatuwaui tunawaombea,” alisema Dk Malasusa.
Aliongeza kuwa wapo wasaliti wa aina nyingi wakiwemo wa ndani ya kanisa, nje ya kanisa, serikalini, ndani ya familia lakini dawa yao sio kuwaadhibu bali ni kuwaombea kwa Mungu ili atende miujiza ndani ya mioyo yao waache usaliti na kuwa watu wema.
Mkoani Ruvuma ambako Ibada ya Ijumaa Kuu imefanyika, Jumuiya ya CCT imeiomba serikali kuendelea kudhibiti matendo maovu na ya mmomonyoko wa maadili nchini ikiwa ni pamoja na kudhibiti muda wa uuzwaji wa pombe ili wazazi na walezi wapate muda wa kukaa na familia zao.
Ombi hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa CCT-Ruvuma, Mhashamu Askofu Raphael Haule wakati akitoa salamu katika Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa mkoani Ruvuma katika Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi-Tunduru na kuongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Noel Mbalawa.
Katika salamu za CCT, Mhashamu Askofu Haule alisema wazazi na walezi hivi leo baadhi yao hawana muda wa kuzungumza na familia zao kwa kuwa wanatumia muda mwingi kufanya matendo maovu yanayochangia mmomonyoko wa maadili.
“Baadhi ya wazazi na walezi katika jamii hawana muda wa kukaa na kuzungumza na familia zao, muda mwingi unatumika kwenye vilabu vya kuuzia pombe na unywaji mara nyingi umechangia athari katika jamii, mauaji, ulemavu, utoro na maadili kuporomoka, serikali tunaomba iendelee kuingilia kati na kuweka ukomo wa muda wa kuuza pombe usiku,” alisema Askofu Haule.
Alisema kumekuwa na tabia nyingi za ajabu, hivyo CCT na kanisa linakemea na kulaani tabia hizo ambazo sio mila, desturi wala utamaduni wa Mtanzania na kuomba ziondoke kwa sababu ni laana.
Akihubiri katika Ibada hiyo Takatifu, Askofu Mbalawa alisema hivi leo baadhi ya watu hawana hofu ya Mungu na wanaendelea kufanya matendo maovu na yasiyo ya maadili na kusema huku ni kumtukana Mungu.
Akizungumzia kusulubiwa kwa Kristo kuna maana gani hivi leo, Askofu Mbalawa alisema jamii inapaswa kuacha unafiki na kusema katika majira haya ya Kwaresima yawe ya toba ya kweli na iwe dhahiri na safi badala ya kuwa wanafiki.
Alisema Ijumaa Kuu na katika kukumbuka mateso ya Yesu msalabani yaikumbushe jamii kuacha matendo maovu na kutubu ili kujenga jamii yenye upendo, amani na kuacha usaliti baina ya watu katika jamii.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wakiwemo wachungaji, makasisi, wainjilisti na viongozi wengine wa CCT na makanisa mkoani Ruvuma, waumini na wananchi