Rais Samia akutana na viongozi mbalimbali

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan ameongoza kikao cha viongozi mbalimbali wa serikali kinachohusu  kuanza kwa mchakato wa katiba mpya.

Kikao hicho kilianza majira ya alasiri  Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo  Mei 6, 2023.

Tayari Rais Samia ametoa maelekezo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa lengo likiwa ni kuwashirikisha wadau katika kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Advertisement

Kuitisha  kikao hicho cha viongozi wa serikali yake ni utekekezaji wa ahadi aliyoitoa katika siku ya Wanawake Duniani Machi 8,2023 akihutubia kwenye Baraza Kuu la Wanawake Chadema (Bawacha) mjini Moshi.

Katika mkutano huo Rais Samia alisema hakuna anayepinga katiba mpya na kwamba muda si mrefu ataunda kamati ambayo itashirikiana na vyama vya upinzani.

“Swala katiba hakuna anayekataa hata chama changu hakuna anayekataa, na muda si mrefu tutatangaza kamati ambayo itashughulikia jambo hilo”.Alisema  Rais Samia.

Mbali mchakato wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi, zikiwemo Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *