Watatu mbaroni kukwamisha sensa Musoma

WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi  kwa kujaribu kukwamisha Sensa ya Watu na Makazi mjini Musoma.

Mratibu wa Sensa wa Manispaa ya Musoma, Joseph Ochora amemtaja karani wa sensa, Thomas Ndyetabura kwamba anashikiliwa na polisi tangu juzi  kwa kuhesabu kaya moja tu kutwa nzima, baadaye kukutwa akiwa amelewa.

Kwa mujibu wa Ochora karani huyo alitakiwa kuhesabu kaya kati ya 20 hadi 30 kwenye Kata ya Kwangwa, lakini baada ya matendo hayo nafasi yake ikatolewa kwa karani mwingine na kazi inaendelea.

“Changamoto nyingine imetokea Kata ya Kitaji, Barabara ya Shaban Nyumba Namba 28, ambapo kaya moja ilikataa kuhesabiwa,  tumewakabidhi polisi,” amesema Ochora.

Amesema kaya hiyo ina binti aliyemtaja kwa jina moja la Leila na mama yake mzazi (hakumtaja majina), kwamba licha ya kugoma kuhesabiwa, waliwatolea maneno ya kashfa karani wa sensa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Longinus  Tibishubwamu amethibitisha uwepo wa matukio hayo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button