Karani wa sensa Bunda ajifungua, Rorya mambo mazuri

WAKATI Sensa ya Watu na Makazi ikiendelea vizuri katika Wilaya za Bunda na Rorya mkoani Mara, mmoja wa makarani wa sensa hiyo wilayani Bunda amejifungua mtoto usiku wa kuamkia leo.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Nassary amesema Mmoja kati ya makarani zaidi ya 1, 000 amejifungua mtoto usiku wa kuamkia leo, hivyo idadi ya watu waliohesabiwa wilayani humo, imeongezeka.

Amesema mpaka wakati akizungumza, tukio hilo lilikuwa changamoto pekee   ingawa kwa upande mwingine ni baraka inayowaongezea sababu za kushukuru Mungu.

“Alipojifungua, kwa kuwa tunao makrani wa akiba, mmoja akachukua nafasi, kazi zinaendelea,” amesema Nassary.

Amewaondoa wasiwasi wanaompigia simu wakisema hawajahesabiwa, kwamba hakuna mwana Bunda atakayeachwa bila kuhesabiwa, waendelee kutoa ushirikiano kama wanavyofanya tangu kazi hiyo ilipoanza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma  Chikoka amesema licha ya wakazi wengi kuishi visiwani kutokana na asilimia 77 ya Wilaya hiyo kuzungukwa na Ziwa Victoria, sensa inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi.

“Mpaka sasa nimefuatilia maendeleo ya kazi hii katika Visiwa vya Ngoche kitongoji cha Ngoche, Bugambwa kitongoji cha Keumbe katika Kijiji cha Mkengwa na Kisiwa cha Ryamkaba Kata ya Nyamunga, mambo yapo vizuri sana,” amesema Chikoka maarufu  Mchopanga.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamewataka wananchi ambao hawajafikiwa, pindi wanapoondoka nyumbani waache taarifa walizoziandaa kwa ajili ya kushiriki sensa, ikiwamo namba ya simu ili kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button