Kardinali Pengo azuru kaburi la JPM

Kardinali Pengo azuru kaburi la JPM

KATIKA kumbukizi ya miaka miwili ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo amezuru Chato na kutembelea kaburi la kiongozi huyo aliyefariki Machi 17, 2021.

Akizungumuza jana na waandishi wa habari akiwa ofisi ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Kardinali Pengo alisema amefanya hivyo kwani hakupata fursa hiyo wakati wa mazishi ya Dk Magufuli.

“Nimechukua nafasi hii kwenda kutoa heshima kule Chato, kwenye kaburi la yeye aliyezoea kuniita mimi baba yake, mimi nilipenda kumuita zaidi rafiki yangu, Dk John Pombe Magufuli.

Advertisement

“Sikuweza kufika wakati ule wa mazishi, kwa sababu hali yangu ya afya haikuwa nzuri, na nilipoweka dhana kujaribu kufika kwenye mazishi, niliambiwa tu na madaktari kwamba wewe unataka kuleta msiba juu ya msiba.

“Ili kuepusha hilo, basi nikabaki kule Dar es Salaam, na muda wote nimekuwa nikitamani kukutana na mama Janeth Magufuli,” amesema na kuongeza kuwa:

“Nilikutana naye mara baada ya kifo cha John (Magufuli), lakini nilikuahidi kwamba siku moja nitafika kutoa heshima zangu kwa kaburi lake Dk John Magufuli.”

Amesema ametimiza ahadi hiyo kwani imekuwa ni rehema kipindi hiki cha kumbukizi ya miaka miwili ya kifo cha Hayati Dk Magufuli kimeambatana na baraka ya kutabaruku Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Geita lililovamiwa na kuharibiwa hivi karibuni.

Kardinali Pengo anatarajiwa kuongoza ibada maalum ya kutabaruku kanisa hilo itakayofanyika Jumamosi Machi 18, 2023, ili kutoa fursa ya kanisa hilo kuanza kutumika tena kwa ajili ya ibaada.