Karibu Kamala Harris tudumishe ushirikiano

MAKAMU wa Rais wa Marekani, Kamala Harris anatarajiwa kuwasili nchini leo kwa ziara ya siku tatu.

Kamala ambaye ni mwanamke wa kwanza katika historia ya Taifa la Marekani kushika wadhifa huo, anatarajiwa kuwasili nchini akitokea Ghana akiwa katika ziara ya mataifa matatu ya Afrika ambayo itamfikisha pia Zambia.

Anakuja nchini kwa mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kama Kamala, alikuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania kuwa Makamu wa Rais, na pia ameweka historia nyingine kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika taifa letu.

Kamala anaitembelea Tanzania na mataifa hayo mengine ya Afrika ikiwa ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa Marekani tangu utawala wa Rais Joe Biden uingie madarakani.

Kwa hiyo, ziara yake nchini ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani na matokeo ya juhudi za Rais Samia kukuza na kuimarisha diplomasia na ushirikiano wa kimataifa tangu aingie madarakani.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, ziara hii muhimu pamoja na mambo mengine, inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani hususani kwenye maeneo ya kimkakati kama vile biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji mazingira.

Tax amebainisha kuwa Marekani imechangia kwa kiasi kikubwa uwekezaji nchini kwa kuwa na miradi 266 iliyosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4,778.6.

Aidha, amesema sekta ya utalii inaongoza kwa uwekezaji wa Marekani nchini kwa jumla ya miradi 68, ikifuatiwa na sekta ya uzalishaji viwandani yenye miradi 66.

Kwa mujibu wake, miradi hii imetengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania. Kwa hiyo, Marekani na Tanzania zina uhusiano mzuri wenye tija kwa pande zote.

Katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano huu kati ya Marekani na Tanzania, Desemba mwaka jana, Rais Samia alikuwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliokutana na Rais Biden jijini Washington, D.C na kuzungumza naye masuala kadhaa kuhusu ushirikiano kati yao.

Ni kutokana na mwendelezo huo na uhusiano mzuri, Makamu wa Rais Kamala anaitembelea Tanzania kudumisha na kuendeleza kuona fursa za kuimarisha ushirikiano katika nyanja hizo zilizotajwa hapo juu na nyingine kwa manufaa ya mataifa haya mawili.

Tunaamini ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani itakuwa chachu ya kuendeleza uhusiano huu mzuri na pia kuzidi kufungua fursa za biashara kwa pande zote mbili.

Tanzania inajivunia kuwa mshirika wa Marekani katika maendeleo kutokana na miradi yake katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, hiyo ziara ya Kamala Harris ni kielelezo cha uhusiano huo mzuri.

Hivyo, tunawaomba wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumlaki mwanamama huyu mwenye historia ya kuvutia ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika.

Karibu Tanzania Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris. Jisikie nyumbani.

Habari Zifananazo

Back to top button