Kasi ya umalizaji mashauri yafikia 84%

MSAJILI Mkuu Mahakama ya Tanzania, Wilbert Chuma amesema kasi ya umalizaji wa mashauri kwa kipindi cha miaka miwili ya awamu ya serikali ya 6 imeongezeka hadi asilimia 84 kwa mwaka 2022 kutoka asilimia 74 kwa mwaka 2021.

Amesema ongezeko hilo ni pamoja na usikilizaji, umalizaji wa mashauri na utoaji haki kwa ujumla.

Chuma alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumza kwenye kipindi cha Sema na Mahakama katika mada ya kuangalia hali ya utoaji na upatikanaji haki na matumizi ya Tehama kwa kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema utoaji haki unaanza pindi shauri linapokuwa limefunguliwa hadi linapomalizika kwa kuangalia kama mahakama inafuata taratibu wakati wa uendeshaji wake.

Alisema bado wanaendelea kuhakikisha hakuna kasi ya mrundikano wa mashauri katika ngazi zote za mahakama na kwa kuweka vikao mahususi vya kuondokana na mrundikano.

“Tumeweza kupunguza mrundikano kutoka asilimia 11 ya mrundikano wa mashauri 53,864 kwa mwaka 2021 mpaka asilimia 5 ya mashauri kwa mwaka 2022 kwa kushirikiana na wadau bado tunaendelea kuweka mikakati ya mifumo thabiti ya kuona jinsi ya kuondoa na kumaliza mrundikano wa mashauri mahakamani,” alisema Chuma.

Kwa upande wa Tehama, Msajili alisema imewasaidia kwa kiasi kikubwa kwa sababu wamefikia asilimia 99 ya ufunguaji wa mashauri kupitia mtandao ndani ya saa 24.

Alisema imesaidia katika usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao kwa washitakiwa waliopo ndani mfano katika mahakama ya kisutu.

“TEHAMA imerahisisha upatikanaji wa taarifa za kimahakama kwani kwa sasa mtu anaweza kwenda kwenye mtandao na kujifunza mambo mbalimbali ya mahakama tofauti na hapo awali tulipokuwa mpaka tukusanye taarifa ya kila kanda ndio tuziweke pamoja,” alisema.

Pia alisema imesaidia kurahisisha upatikanaji wa nakala ya hukumu mara tu baada ya hakimu kumaliza kutoa hukumu inapandishwa kwenye maktaba mtandao hivyo husaidia mtu kupata nakala yake ya hukumu kwa haraka ambapo mpaka sasa wamepandisha nakala za hukumu 18,079 kwa mahakama kuu na ya Rufani.

Alisema wamewapatia majaji kompyuta mpakato ili kuwawezesha kupandisha hukumu zao kwenye Maktaba mtandao wakati hapo awali mtu alikuwa anasubiri nakala ya hukumu mpaka siku 21 baada ya kuhukumiwa.

Akizungumza na madalali wa mahakama kwenda kutoa vitu nje ili kufanya mnada, Msajili alisema ni takwa la kikatiba na kwenye usuluhishi dalali hayupo ila huwa anaingia wakati usuluhishi umemalizika na kutekeleza haki kwa upande utakaokuwa umeshinda.

“Ni vyema ikafahamika kwamba dhana hii ya usuluhishi ni takwa la kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 107 (A) ibara ndogo ya pili (d) ambayo inasisitiza juu ya upatanishi katika mashauri mbalimbali ndio maana kama mtu hajaridhika rufaa zipo wazi na itabidi afuate sheria,” alisema Chuma.

Aliwataka wananchi kumaliza migogoro yao kwa njia ya usuluhishi kabla ya kufika mahakamani ili kumaliza chuki, gharama pamoja na mrundikano wa mashauri, kuokoa muda wa kufanya shughuli nyingine ili kukuza uchumi

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x