Kasiga kuwania uenyekiti wa gofu

Mchezaji maarufu wa klabu ya Lugalo, Gilman Kasiga

UCHAGUZI mkuu wa chama cha gofu Tanzania (TGU) umepamba moto baada ya mchezaji maarufu wa klabu ya Lugalo, Gilman Kasiga kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Mwenyekiti.

TGU kimepanga kufanya uchaguzi Oktoba 6 kwenye klabu ya Gymkhana ya mkoani Morogoro.

Pia mchezaji wa timu ya gofu ya Gymkhana Arusha Pridence  Kaijage amechukua fomu ya kugombea nafasi ya makamu Mwenyekiti.

Advertisement

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Kasiga alisema sababu kubwa ya kuwania nafasi hiyo ni kuleta maendeleo makubwa ya mchezo huo akianisha maeneo makuu matatu.

Kasiga alisema kuwa eneo la kwanza ni kuendeleza mchezo wa gofu kwa vijana ili kuwa na nyota wapya baada ya kizazi kilichopo kuacha kucheza na pili kuwazesha watu wazima kujiunga na mchezo ikiwa sehemu ya kuimarisha mtandao miongoni mwao.

“Lengo la tatu ni kuimarisha wachezaji wa gofu wa kulipwa ambao kimsingi ndio makocha wa wachezaji wa sasa, vijana na watu wazima,” alisema.

Alisema kuwa uongozi wake utazingatia misingi yote ya utawala bora, uadilifu, uwazi, nidhamu na masuala mbalimbali ambayo yatawavutia wadau ikiwa ni pamoja na kampuni kudhamini mashindano mbalimbali,” alisema Kasiga.