Kaskazini Unguja mabingwa mbio za Wanawake

MKOA wa Kaskazini Unguja umeibuka kidedea katika Mashindano ya Wanawake ya Riadha ya Ladies First yaliyomalizika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana.

Kaskazini Unguja walitangazwa mabingwa wa jumla baada ya kujizolea medali tano za dhahabu na moja ya fedha wakati Arusha walishika nafasi ya pili baada ya kutwaa medali nne za dhahabu na nne za shaba.

Mkoa wa Pwani, wenyewe umeshika nafasi ya tatu ukiwa na medali tatu za fedha na moja ya shaba, huku Kusini Unguja ukimaliza katika nafasi ya nne baada ya kunyakua medali mbili za fedha na shaba mbili, Mara umekuwa wa tano baada ya kutwaa medali mbili za fedha.

Tanga wa sita baada ya kupata medali moja ya fedha, huku Kilimanjaro na Mjini Magharibi zikishika nafasi ya saba na nane.

Mashindano hayo ya nne yalishirikisha jumla ya mikoa 30, huku mkoa wa Songwe ndio pekee ukishindwa kupeleka mchezaji hata mmoja.

Katika mchezo wa fainali ya meta 200 jana, Kaskazini Unguja walitamba baada ya kushika nafasi tatu za kwanza wakiongozwa na Winfrida Makenji aliyetumia sekunde 24.10, Jane Maige alimaliza wa pili kwa sekunde 24.41 na Thereza Bernad alikuwa watatu kwa sekunde 25.86.

Katika mbio za meta 100, Makenji alimaliza wa kwanza kwa kutumia sekunde 11.31, Siwema Julius wa Pwani alimaliza wa pili kwa sekunde 12.68 na bertha Evarist wa Kilimanjaro alishika nafasi ya tatu kwa sekunde 12.94.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha ametoa wito kwa vyama vya michezo vya mikoa na Shirikisho la kitaifa kufanya mashindano ya mara kwa mara kuwasaidia wachezaji, kwani Tanzania ina kiu ya kufanya vizuri na kupata medali za kimataifa.

Pia, aliwasihi wachezaji kutoishia kwenye mashindano hayo bali kuendelea kutenga muda wa kufanya mazoezi ili waweze kufikia ndoto zao na kutengeneza kipato kitakachowasaidia kuendesha maisha yao.

 

Habari Zifananazo

Back to top button