Kata ya Kamundi wamshukuru Samia ujenzi wa daraja

Kata ya Kamundi wamshukuru Samia ujenzi wa daraja

WAKAZI wa Kata ya Kamundi Halmashauri ya Nanyumbu, mkoani Mtwara, wamepanga kufanya sherehe ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajengea daraja katika kata hiyo, jambo ambalo wananchi hao wanadai lilishindikana kwa awamu zilizotangulia.

Wamesema sherehe hizo watazifanya wakati wa uzinduzi wa daraja hilo liitwalo Mkoromwana lenye thamani ya sh milioni 82.

Wakizungumza na waandishi wa habari, waliotembelea daraja hilo, wananchi hao wamesema daraja  lilishindikana kujengwa tangu awamu ya kwanza ya serikali licha ya kuwa lilikuwa linajaa maji kipindi cha masika na kusababisha adha kubwa kwa wananchi ,ikiwemo vifo.

Advertisement

“Tunaweza kusema hili daraja ni la Mbunge wetu Mhata, wabunge wengine tulikuwa tunawaeleza wanasema kwamba hapa hela yake ‘kwechiwekichi’ yaani kwamba hela ni nyingi sana, serikali haiwezi kutoa, lakini Mheshimiwa Mhata ameingia tumemueleza amepeleka ombi letu kwa Rais na ametujengea,” amesema Ahmed Kinde (70) Mzee wa Kijiji Cha Kamundi.

Mzee huyo amesema kwa sasa wana furaha na kwamba wanataka kuandaa sikukuu kumshukuru Rais.

“Yani tuna furaha kila saa ni furaha, tunataka kutengeneza sikukuu kumshukuru Mheshimiwa Rais,” amesema.

Amesema kabla ya kujengwa daraja hilo, wananchi walikuwa wanapata adha kubwa hasa kipindi cha mvua, ambapo wamama wajawazito pamoja na wanafunzi wa Shule walikuwa wanapata shida kubwa na hata wakati mwingine kusombwa na maji.

Akielezea zaidi, Mzee Kinde amesema jina la daraja hilo (Mkoromwana) lilitokana na athari walizokuwa wanazipata wananchi hao, wakati wakivuka hasa akina mama wajawazito, ambao wengine walipoteza maisha kwa kusombwa na maji wakati wakivuka kwenda  kijiji jirani kufuata zahanati kwa ajili ya kujifungua.

“Adha ni ya siku nyingi, ni kwamba jina la daraja hili Mkoromwana, ambalo ni jina la kilugha kwa Wamakua, lina maana mto huu umesomba mama na mtoto, Mkoro ni mama na mwana ni mtoto wake.

“ Ilikuwa ni shida kweli kwa akina mama wajawazito kuvuka huo mto kwenda kupata huduma,” amesema.

Kinde amesema kuwa ilikuwa ni shida kubwa pia kwa wanafunzi kufaulu, kwa sababu walilazimika kukaa nyumbani kipindi chote cha mvua.

 

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Kamundi, wakizungumza na waandishi wa habari (Picha na Anne Robi).

“Watoto walikuwa hawasomi, mto ukijaa hawaendi shule, vifo vingi vilikuwa vinatokea,” amesema.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kamundi, Suzan Nampeshe, amesema ujenzi wa daraja hilo kwa sasa umewarahisishia usafiri na kwamba muda wowote daraja hilo linapitika na kuwawezesha wananchi kupata huduma zao, ikiwemo huduma za afya kiurahisi.

‘Kwa sasa hivi tunashukuru Mheshimiwa Rais  Samia Suluhu kwa kweli ametugusa, ametusaidia sana kutujengea hili daraja, maana  ameturahisishia usafiri, sasa hivi ni uhakika muda wowote na saa yoyote, tunapata huduma kwa uhakika,” amesema.