Kata ya Maboga walia na ubovu wa barabara

WANANCHI wa kata ya Maboga wilayani Iringa wanakabiliwa na adha ya ukosefu wa huduma ya usafiri wa abiria baada ya barabara yao inayowaunganisha na kata ya Wasa na Kalenga kuharibiwa kwa kiwango cha kutopitika na mvua zinazoendelea kunyesha.

Pamoja na mvua hizo, mkandarasi aliyepewa tenda ya kuitengeneza barabara hiyo ya urefu wa kilometa 24, Boimanda Modern Construction Ltd amesitisha kuendelea na ujenzi wake jambo linalozidisha athari kwa wananchi wanaoitegemea kwa shughuli zao mbalimbali za kijamii na maendeleo.

Barabara hiyo inayosimamiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Iringa ilianza kutengenezwa kwa vipande vipande na mkandarasi huyo, Oktoba mwaka jana kabla ya ujenzi wake unaotakiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei, mwaka huu kusimama Januari, mwaka huu.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Makongati katika kata hiyo ya Maboga, Emmanuel Sanga alisema wanalazimika kukodi pikipiki kwa gharama kubwa kwa ajili ya kufuata huduma na bidhaa mbalimbali nje ya kata hiyo.

“Lakini shida kubwa ni pale wananchi wanapotaka kupeleka bidhaa zao za kilimo kama mahindi mabichi sokoni mjini Iringa kwa ajili ya kuuza. Hakuna gari kubwa linaweza kuja kwasasa katika kata yetu hii kwasababu ya kadhia hii ya barabara,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Kiponzero, Allen Dallu alisema ubovu wa barabara hasa katika kipindi cha mvua ni changamoto inayoisibu kata hiyo kwa miaka yote na akawaomba TARURA waangalie uwezekano wa kujenga kwa kiwango cha lami au zege hasa katika maeneo korofi zaidi.

Diwani wa kata hiyo Veni Muyinga ameishushia lawama TARURA akisema inafahamu changamoto ya barabara hiyo lakini haitaki kuchukua hatua za kudumu ili kuwaondolea taharuki wananchi kila msimu wa mvua unapokaribia au kuanza.

Akimzungumzia mkandarasi huyo, Muyinga alisema baada ya kufika katika eneo la mradi rekodi zao zinaonesha alifanya kazi kwa siku 14 tu kabla ya kusitisha ujenzi huo aliouanzia Kalenga kuelekea Weru bila taarifa yoyote kutolewa kwa wananchi.

Alisema kata ya Maboga ni miongoni mwa kata zinazotegemewa kwa uzalishaji mkubwa wa mahindi mabichi pamoja na malimbichi nyinginezo hivyo barabara hiyo ni muhimu kwa ajili ya kuinua na kukuza uchumi wa wananchi wake na Taifa kwa ujumla.

“Kama kuna sababu iliyomkimbiza Mkandarasi tuwaombe TARURA wenyewe waje na wachukue hatua za dharula kudhibiti maeneo yaliyoharibika zaidi ili shughuli za usafiri ziweze kuendelea kwani wanaoathirika na kadhia hiyo ni wananchi, wangu,” alisema.

Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Iringa Vijijini ikiongozwa na Katibu wa Chama hicho Gama Juma Gama imemnyoshea kidole Mkandarasi huyo ikisema hatua yake ya kuondoka katika eneo la mradi bila kutoa taarifa ni dharau kwa wananchi na serikali iliyotoa kodi zao ili kuimarisha barabara hiyo.

“Tunawaomba TARURA wafanye uchunguzi kubaini sababu ya kukwama kwa ujenzi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kuwanusuru wananchi wetu na kadhia wanayopata,” alisema Gama.

Mwakilishi wa Meneja wa TARURA wilaya ya Iringa, Adelick Theonest amejibu malalamiko hayo akisema mvua zinazoendelea kunyesha ndizo ambazo zimesababisha ujenzi wa barabara hiyo usitishwe.

Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh Milioni 400 kwa ajili ya ukarabati wa barabara hiyo unaotarajiwa kuendelea wakati wowote kuanzia sasa..

Habari Zifananazo

Back to top button