Kata ya Nsemulwa walia changamoto ya maji

WANANCHI wa Mtaa wa Mnazi Mmoja, Kata ya Nsemulwa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, wameomba serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Suluhu Hassan iwasaidie kutatua changamoto ya maji eneo lao.

Wakizungumza na HabariLeo wakiwa katika mto wanaoutegemea kwa matumizi mbalimbali, wananchi hao wamesema eneo lao halina huduma ya maji safi na salama.

Wamesema maji wanayotumia kwa sasa si salama, kwa kuwa wanachota mtoni, huku wakichangia na wanyama sanjari na kufanyia shughuli mbalimbali za kibinadamu, ikiwemo kilimo, hali inayosababisha kuugua homa za tumbo.

“Maisha tunayoishi ni magumu sana, tunaugua ovyo, mjukuu wangu ameugua kuharisha na kutapika kwa sababu ya maji haya,” amesema Haika Damiano mkazi wa mtaa huo.

Wakijibu malalamiko hayo, Mhandisi Helman Nguki na Mhandisi Eddo Richard kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mpanda(MUWASA), wamesema si wananchi wa mtaa huo wanaopitia changamoto ya maji, bali maeneo mengi bado hayajafikiwa huduma ya maji na tayari yamo kwenye mpango wa mwaka wa fedha 2022/2023.

Hivi karibuni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi katika ziara yake wakati akijibu kero za wananchi kuhusu changamoto za maji, alisema Wizara ya Maji imeongezewa fedha kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji maeneo mbalimbali.

 

Habari Zifananazo

Back to top button