Kata ya Uhambingeto yapatiwa maji

WAKALA wa Maji na usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) Mkoa wa Iringa imetekeleza agizo la Waziri wa Maji, Juma Aweso lililowataka kuhakikisha mradi wa maji wa Uhambingeto wilayani Kilolo mkoani Iringa unakamilika na kuanza kutoa huduma kwa Wananchi.

Kukamilika kwa mradi huo kumekuja baada ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa,  Daniel Chongolo katika ziara yake aliyofanya Mei mwaka huu kata ya Uhambingeto kupokelewa na vilio vya wananchi kuhusu kero ya maji na kusuasua kwa mradi huo.

Katika kuipatia ufumbuzi kero hiyo Chongolo alimpa siku 10 Waziri wa Maji Juma Aweso kuhakikisha suluhu ya changamoto hiyo inapatikana.

Akijibu kilio cha Wananchi wa kata hiyo, Aweso aliomba radhi na akaahidi kutumia miezi mitatu toka Juni mwaka huu ili wizara yake izifanyie kazi dosari zilizojitokeza na kuukamilisha mradi huo ili wananchi waanze kupata maji.

Kukamilika kwa sehemu kubwa ya mradi huo kumepeleka shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan na furaha kwa wananchi zaidi ya 8,989 wa kata na kijiji cha Uhambingeto kwa kuondokana na adha ya ukosefu wa maji safi na salama kwa zaidi ya miaka 60.

Zaidi ya Sh bilioni 1.7 kati ya Sh bilioni 2.1 zilizokuwa zimetengwa zimetumiwa na Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA) kufikishia huduma ya maji katika eneo hilo kupitia chanzo cha milima ya Selebu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi RUWASA Mhandisi Ruth Koya ametembelea eneo hilo na kuipongeza RUWASA Mkoa wa Iringa kwa hakikisha mradi huo uliokwama kakamilika Januari mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa, umekamilika na umeanza kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, Rehema Kikoti alisema historia imeandikwa katika kijiji hicho baada ya kuanza kupata huduma ya maji ya bomba ambayo hawakuwa nayo kwa zaidi ya miaka 60 ya Uhuru.

“Kabla ya mradi tulikuwa tunafuata maji umbali mrefu kwenye mito na madimbwi ambayo nayo ikifika mwezi wa nane yanakauka kwasababu ya jua kali na uharibifu wa mazingira na hivyo kuongeza adha kwa wananchi,” alisema.

Alisema kukauka kwa maji ya mito na madimbwi kulikuwa kunawalazimu kununua maji katika vijiji jirani vya Kipaduka na Vitono kwa kati ya Sh 2,000 na Sh 5,000 kwa dumu la lita 20 na hivyo kuongeza gharama za maisha kwa wananchi.

“Tunaishukuru sana serikali ya Mama Samia kwa mikakati yake inayolenga kumtua mama ndoo kichwani. Kijijini hapa sasa ni furaha isiyo na kifani hasa kwa wanawake waliokuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji,” alisema.

Akipokea shukrani hizo kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Maji Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi RUWASA alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ina nia ya dhati ya kumtua mwanamke ndoo kichwani kwa kusogeza huduma ya maji safi na salama kwa umbali usiozidi mita 400.

“Mradi huu ambao kila kitu chake kitakuwa kimekamilika kwa asilimia 100 Septemba 30 mwaka huu tayari umeanza kutoa huduma kwa baadhi ya vijiji vya Kata hii ya Uhambingeto; niwaombe muendelee kuiunga mkono serikali kwani ina nia ya dhati ya kufikisha huduma huduma mbalimbali kila mahali walipo wananchi,” alisema Mhandisi Koya.

Aliwataka wananchi hao kuwa walinzi wa kwanza wa miundombinu ya maji kijijini hapo ili iwe na manufaa kwa kijiji chote.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi wiwani wa kata Uhambingeto Tulinumtwa Alphonce alisema zile zaidi ya kilometa tisa walizokuwa wakitembea kutafuta maji zimefika ukomo.

“Kilio chetu cha miaka yote kimepatiwa ufumbuzi, hatua inayofuata ni kwa wananchi kuunganisha huduma ya maji katika nyumba zao. Uhambingeto inaenda kuwa mjini baada ya kufikiwa na huduma hii,” alisema.

Diwani huyo aliwapongeza mafundi wanaotekeleza mradi huo kwa moyo wa uzalendo na wa kujituma uliowawezesha kukamilisha mradi huo kwa asilimia kubwa.

“Wamefanya kazi usiku na mchana bila kuchoka. Tunaomba Serikali imuangalie kwa Jicho la pekee huyu Mhandisi Kilave kwani yeye hajaajiriwa lakini amesimamia mradi huu kwa uadilifu hadi umeanza kutoa huduma hata kabla ya muda wa kwenye Mkataba kumalizika,” alisema diwani huyo.

Habari Zifananazo

6 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button